UTALII WA UTAMADUNI WARINDIMA MOROGORO

.......

Na Sixmund Begashe, Morogoro

WATANZANIA wameendelea kunufaika na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni 2026 kwa kupata elimu maridhawa ya utalii wa utamaduni nchini. 

Akizungumza na mamia ya wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye tashama hilo mkoani Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Adam Malima, amewasisitiza wananchi kutumia nafasi hiyo katika kujipanga vyema na mazao ya utalii wa utamaduni kwa wageni watakaokuja nchini kwenye Michuoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. 

Mhe. Malima amebainisha kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa mazao ya utalii hususan Mkoa wa Morogoro ambao umepakana na Hifadhi za Taifa hivyo ni vyema wananchi wakautumia utajiri huo kwa manufaa ya Taifa na mtu mmoja mmoja. 

Akizungumzia ushiriki wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Afisa Utamaduni Mkuu wa TTB, Bi. Gertrude Ndalo amesema lengo ni kukutana na wadau wa utamaduni ili kuendelea kutoa elimu ya fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii kupitia utamaduni. 

Aidha, Bi. Ndalo ameongeza kuwa, wanalitumia tamasha hilo kuhamasisha utalii wa ndani ili Watanzania wanufaike na vivutio vyao. 

Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii zilizo shiriki katika tamasha hilo lenye mvuto mkubwa kwa watalii wa ndani na nje, ni pamoja na TTB, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzani (TFS), Mamlaka ya Bonde la Ngorongo (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT).



 

0/Post a Comment/Comments