CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeonesha namna elimu, ujuzi na ubunifu vinavyoweza kugeuzwa kuwa suluhisho la changamoto za maendeleo, kupitia teknolojia mbalimbali zinazolenga sekta za ujenzi, barabara, maji na nishati.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu jijini Tanga, Agosti 16, 2026, Mtafiti wa Kemia kutoka UDSM, Dkt. Makungu Madirisha, amesema chuo hicho kimewasilisha bunifu mbalimbali, zikiwemo Novacem, teknolojia ya saruji mbadala inayotumia malighafi zinazopatikana nchini kutengeneza matofali, paving na paneli nyepesi za ujenzi.
Amesema Novacem inawezesha uzalishaji wa matofali mepesi kwa ajili ya majengo ya ghorofa na paneli zinazosaidia kuzuia joto kuingia ndani ya majengo, huku bidhaa hizo zikiwa na uimara na kustahimili fangasi pamoja na kemikali.
Dkt. Madirisha amesema UDSM pia imebuni Duracem kwa ajili ya ujenzi wa barabara, hasa katika maeneo yenye unyevunyevu na maji mengi, pamoja na Duracem 1A inayoweza kutumika pamoja na lami baridi.
Aidha Amesema teknolojia hizo zinalenga kuongeza uimara wa barabara na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa lami.
Pia meongeza kuwa bunifu nyingine ni Bentocem TZ kwa ajili ya uchimbaji wa visima vya maji na Flacem inayotumika kusafisha biogesi kwa kuondoa viambata visivyohitajika na kuongeza ubora wa biometani. Hata hivyo, amesema mahitaji ya bidhaa hizo ni makubwa kuliko uwezo wa sasa wa uzalishaji kutokana na ukosefu wa mashine ya Flash Calciner yenye thamani ya takribani dola 200,000.
Dkt. Madirisha amezitaka taasisi kama TARURA, PURA na Wizara ya Nishati kuunga mkono na kutumia teknolojia zinazozalishwa na wataalamu wazawa, akisema hatua hiyo itasaidia kukuza ubunifu wa ndani, matumizi ya malighafi za Tanzania na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




Post a Comment