WATAFITI ZAIDI YA 14 KUTOKA CHUO CHA UDSM WAPATIWA TUZO

........

Na Ester Maile TANGA 

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeonyesha mafanikio katika tafiti na uchapishaji wa machapisho ya kitaaluma, baada ya watafiti zaidi ya 14 wa chuo hicho kutambuliwa na kutunukiwa tuzo kwa machapisho yao yaliyochapishwa katika majarida ya kimataifa yenye hadhi na kutambulika katika mifumo ya kimataifa ya utafiti.

Tuzo hizo zimekabidhiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Agosti 18, 2026, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu. 

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayeshughulikia masuala ya Utafiti, Prof. Nelson Boniface, amesema chuo hicho kinajivunia ubora wa tafiti na machapisho yanayozalishwa na watafiti wake.

Prof. Boniface amesema asilimia 52 ya machapisho ya watafiti wa UDSM yanachapishwa katika majarida ya kimataifa yenye viwango vya juu, yakiwemo yaliyo katika kundi la Q1, pamoja na yale yanayotambuliwa katika Web of Science na Scopus, huku baadhi yakichapishwa kupitia wachapishaji wakubwa wa kimataifa kama Elsevier. 

Amesema ukuaji wa machapisho katika majarida hayo umefikia asilimia 16, hali inayoonyesha kuongezeka kwa ubora na ushindani wa tafiti zinazozalishwa na chuo hicho.

Ameeleza kuwa tafiti zilizotambuliwa kupitia tuzo hizo zimejikita katika maeneo mbalimbali, ikiwemo afya, sayansi asilia kama hisabati na fizikia, pamoja na uhandisi. 

Tafiti hizo zimeelekezwa katika kutafuta maarifa na suluhisho za changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii na sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa Prof. Boniface, kutambuliwa kwa watafiti hao ni ishara ya mchango unaotolewa na UDSM katika uzalishaji wa maarifa kupitia tafiti zenye viwango vya kimataifa. 

Amesema mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha nafasi ya chuo hicho katika kufanya utafiti na kuzalisha machapisho yenye mchango katika kutatua changamoto za maendeleo, hususan katika nyanja za afya, sayansi asilia, biolojia na uhandisi.


 

0/Post a Comment/Comments