WAZIRI KIJAJI AAGIZA KITUO CHA ASKARI WA UHIFADHI KIJENGWE KARAGWE KUDHIBITI UVAMIZI WA TEMBO.


******

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameiagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Askari wa Uhifadhi wilayani Karagwe, ili kudhibiti uvamizi wa tembo unaosababisha uharibifu wa mazao na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Waziri Dkt. Kijaji ametoa maelekezo hayo kufuatia ombi la Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, kuhusu changamoto ya uvamizi wa tembo ambao wamekuwa wakiharibu mazao na kusumbua wananchi wa kata za Rugu, Rugera, Kihanga, Nyakabanga na Nyakakika mara kwa mara.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyakabanga, Dkt. Kijaji alikubali ombi la kujengwa kwa kituo cha mwitikio wa haraka katika kata ya Nyakabanga sambamba na kupeleka ndege nyuki kutokana na kituo kilichopo sasa kuwa mbali na makazi yao jambo linalosababisha askari wanyamapori kufika eneo la tukio kwa kuchelewa.

Kuhusu kifuta jasho na kifuta machozi, Dkt. Kijaji amewaahidi wananchi hao kuwa ndani ya wiki moja kutoka sasa malipo yao yatakuwa yamewafikia wananchi hao.

Katika hatua nyingine, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Nyakakika na kueleza kuwa Serikali tayari imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, na itaongeza shilingi milioni 250 nyingine kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ili kukamilisha mradi huo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, alimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha wakulima wa Wilaya ya Karagwe na Mkoa wa Kagera kuendelea kunufaika na zao la kahawa kupitia bei nzuri ambayo imekuwa ikiongezeka kila msimu.

Bashungwa akizungumzia changamoto ya Barabara ya Nyakahanga–Nyabiyonza–Nyakakika hadi Bweranyange, amesema barabara hiyo yenye urefu wa km 96 ni ya changarawe, huku maeneo korofi yakiwa tayari yamewekewa lami, amesema awali barabara hiyo ilikuwa ikitengewa shilingi milioni 150 kupitia TARURA, lakini sasa imepandishwa hadhi na itasimamiwa na TANROADS, ambapo imetengewa bajeti ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ukarabati.







 

0/Post a Comment/Comments