WAZIRI WA ULINZI AAGIZA KASI KUONGEZWA UJENZI WA SOKO LA MWANGA KIGOMA

*******

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, huku akisisitiza kasi, ubora na matumizi sahihi ya fedha katika miradi hiyo ili wananchi waanze kunufaika kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Waziri Nyansaho amekagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Kisasa la Mwanga, Manispaa ya Kigoma Ujiji, na kutoa agizo la kuongezwa kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Waziri Nyansaho amesisitiza kuwa fedha zinazotumika katika utekelezaji wa mradi huo zinasimamiwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta thamani kwa wananchi.

Amesema mradi huo unafadhiliwa kupitia mkopo wenye ufadhili wa Benki ya Dunia (World Bank), hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kila fedha inayotumika inaleta matokeo chanya na mradi unakamilika kwa wakati.

"Nahitaji kuona mabadiliko ya kweli. Ongezeni nguvu kazi, vifaa na kasi ya utekelezaji ili mradi huu ukamilike ndani ya muda uliopangwa. Huu ni mradi muhimu kwa wananchi na Serikali," amesema Waziri Nyansaho.

Aidha, amewataka viongozi na wasimamizi wa mradi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake na kuwajibika ipasavyo ili kuondoa ucheleweshaji usio wa lazima.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kigoma, Zainabu Katimba, amesema kukamilika kwa Soko la Kisasa la Mwanga kutakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kigoma, hususan kwa wakazi wa Jimbo la Kigoma Mjini.

Amesema soko hilo linatarajiwa kuwa kitovu cha biashara kitakachowawezesha zaidi ya wafanyabiashara 1,000 kufanya shughuli zao katika mazingira bora na salama.

Katimba amesema Serikali ya Awamu ya Sita imelenga kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na biashara inayounganisha Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Zambia.

Aidha, amesema Serikali tayari imeleta meli nne katika Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo, huku hatua nyingine zikiendelea kuongeza ufanisi wa biashara katika ukanda huo.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa.

Amesema kukamilika kwa soko hilo kutachochea ukuaji wa biashara, kuongeza fursa za ajira na kuinua uchumi wa wananchi wa Kigoma, huku manufaa yake yakitarajiwa kufika katika mkoa mzima na nchi kwa ujumla.

 



0/Post a Comment/Comments