Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeeleza mafanikio mbalimbali iliyoyapata kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane 2026, yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026.
Akizungumza wakati wa hafla ya kilele na kufunga maonesho hayo, Afisa kutoka Wizara hiyo, Asia Juma Abdallah, amesema ushiriki wa Wizara umekuwa fursa muhimu ya kuwafikia maelfu ya wananchi na kuwapatia elimu kuhusu huduma za kidijitali, fursa pamoja na manufaa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Kwa mujibu wa Asia, zaidi ya wananchi 3,000 walitembelea banda la Wizara na kupata huduma pamoja na taarifa mbalimbali kuhusu maeneo muhimu ikiwemo usalama mtandao, miundombinu ya TEHAMA, mifumo ya kidijitali na huduma za anwani za makazi.
“Zaidi ya wananchi 3,000 walitembelea banda letu na kupata huduma na taarifa kuhusu shughuli zinazofanywa na idara mbalimbali, ikiwemo usalama mtandao, miundombinu, mifumo ya kidijitali na anwani za makazi,” alisema Asia.
Asia amesema Wizara ina nafasi muhimu katika kusaidia maendeleo ya Taifa kupitia TEHAMA, ikiwa na msisitizo wa kukuza uchumi wa kidijitali nchini sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Ameutaja Mtandao wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Backbone) kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya Wizara, akieleza kuwa umeimarisha mawasiliano na upatikanaji wa huduma za kidijitali serikalini, katika taasisi zake pamoja na kwa wananchi.
Aidha, amesema ujenzi wa zaidi ya minara 750 ya mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umechangia kwa kiasi kikubwa kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini.
Ameeleza kuwa kuimarika kwa mawasiliano kumewawezesha wananchi kutumia zaidi TEHAMA katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, afya na elimu, hivyo kuongeza ufanisi na tija.
Wizara pia imekuwa ikitoa mafunzo kwa vijana na wanafunzi kuhusu matumizi ya drone, roboti na Akili Bandia (AI), kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia zinazoibukia katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Asia amesema teknolojia ya drone, kwa mfano, inaweza kurahisisha shughuli za kilimo na kuongeza ufanisi na tija katika sekta mbalimbali.
Aidha, ameeleza mchango wa mifumo ya kidijitali ya JamiiNamba na JamiiPay katika kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuwezesha miamala, hatua inayochangia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumzia nafasi ya TEHAMA katika kilimo, Asia amesema matumizi ya teknolojia kama Akili Bandia (AI), vihisishi (sensors) na mifumo ya kisasa ya umwagiliaji yana uwezo wa kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi, kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazolikabili sekta ya kilimo.
Aidha, Asia amewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujenga fursa za kiuchumi, badala ya kutumia muda mwingi katika shughuli zisizo na tija.
“Utajiri mkubwa leo unapatikana kupitia mawasiliano. Watu waliounda majukwaa kama Facebook, Instagram na Twitter wamefanikiwa kuwa na utajiri mkubwa. Vijana wetu wasipoteze muda katika shughuli zisizo na tija; watumie vifaa vyao vya TEHAMA kuongeza kipato kupitia biashara za mtandaoni na fursa za kidijitali,” alisema.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Tanzania ina fursa kubwa katika uchumi wa kidijitali, huku akiwataka vijana kutumia ubunifu, teknolojia na mitandao ya kijamii kuanzisha biashara, kutoa huduma na kujiajiri pamoja na kutengeneza ajira kwa wengine.






Post a Comment