Na Mwandishi Wetu, Morogoro
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande ameitaka Bodi ya 13 ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kikamilifu na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Misitu na Nyuki hapa nchini.
Ametoa wito huo leo Septemba 21, 2026 Mkoani Morogoro wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo yenye wajibu wa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na kuisaidia Wizara kutekeleza Sera za Taifa za Misitu na Ufugaji Nyuki.
TAFORI ina jukumu la kusimamia na kuratibu tafiti za kisayansi na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi ya teknolojia bora na uendelezaji wa misitu na ufugaji nyuki hapa nchini ambapo Naibu Waziri Mhe. Chande amesema kuwa Sekta ndogo ya Misitu na Nyuki ina umuhimu mkubwa katika kuchangia pato la taifa, hifadhi ya mazingira na kuongeza ajira kupitia sekta binafsi.
“Mtaungana nami kuwa wadau wa misitu na ufugaji nyuki wanakabiliwa na changamoto ambazo zinahitaji majawabu. Mfano moto wa msituni unaojitokeza na kuathiri ukuaji wa miti, lakini pia upo moto unaoanzishwa katika maeneo ya hifadhi umeleta kero kwa watalii,” amesisitiza Mhe. Chande.
Aidha, amewataka kusimamia tafiti zenye kutoa majibu ya usimamizi, bila kuleta kero kwa watalii, kusaidia kupatikana kwa njia za kutoa taarifa mapema za viashiria vya moto zinazohitajika pia kuhakikisha sampuli za asali inayozailishwa zinapimwa katika maabara zilizopo hapa nchni ili kupunguza gharama na nguvu ya ushindani katika soko la asali nje ya nchi.
“Nchi imepata fursa ya masoko ya asali nje ya nchi hususani soko la Ulaya ambalo lina sharti la kuwasilisha uthibitisho wa maabara juu ya usalama na ubora wa asali yetu, jambo ambalo limekuwa likitulazimisha kupeleka sampuli nje ya nchi, " amesema.
Katika hatua nyingine Mhe. Chande imeitaka Bodi hiyo kuweka mkazo katika kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taasisi wa Miaka Mitano (2026/27 - 2030/31) ili kuhakikisha unazingatia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, kusimamia uwajibijikaji na nidhamu kwa watumishi.












Post a Comment