Utambuzi huo umetolewa kupitia Tuzo za Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), wakati wa Mkutano Mkuu wa Sera wa mwaka 2026 uliofanyika Port Moresby, Papua New Guinea, Septemba 1 hadi 4.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Idara ya Huduma Jumuishi za Fedha wa BoT, Nangi Massawe, alisema Tanzania ilipata Tuzo ya Azimio la Maya kutokana na utekelezaji wa ahadi zake 13 za kuendeleza huduma jumuishi za fedha.
Alisema miongoni mwa hatua hizo ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa Tatu (NFIF 2023–2028), huku ujumuishaji rasmi wa kifedha ukiongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi 76 mwaka 2023.
Massawe alisema matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu pia yamepanda kutoka asilimia 60 hadi asilimia 72 katika kipindi hicho, hatua inayotajwa kuonyesha ongezeko la matumizi ya huduma rasmi za kifedha.
BoT pia ilitambuliwa kupitia Tuzo ya Mafanikio katika Sera za Huduma Jumuishi za Fedha kwa juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa makundi maalumu na yaliyo katika mazingira magumu.
Katika upande wa wanawake, Tanzania ilitambuliwa kwa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Denarau unaolenga kupunguza pengo la kijinsia katika upatikanaji wa huduma za fedha.
Kwa mujibu wa Massawe, mafanikio hayo yamechangiwa na hatua za kisera, udhibiti na teknolojia, ikiwemo matumizi ya mifumo ya Tiered KYC, TIPS na TANQR inayorahisisha upatikanaji wa huduma rasmi za fedha.
Mbali na taasisi, wataalamu wa BoT nao walitambuliwa katika Tuzo za Uongozi wa Kiufundi za AFI, ambapo Massawe alipata tuzo ya Uongozi wa Sera za Huduma Jumuishi za Fedha, huku Dkt. Khadijah Kishimba akitambuliwa kwa Mwenendo wa Soko na Uwezeshaji wa Watumiaji wa Huduma za Fedha.

Post a Comment