DAWA ZA SHILINGI MILIONI 360 ZANASWA AIRPORT YA DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jiji Dar es salaam.
*******

 Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata shehena ya dawa na vifaa tiba visivyosajiliwa yenye thamani ya Sh milioni 360.

Mzigo huo umenaswa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema shehena hiyo imekamatwa kwa awamu mbili.

Amesema mzigo wenye thamani ya Sh milioni 310 ulikamatwa Septemba 7, mwaka huu.

Mzigo mwingine wenye thamani ya Sh milioni 50 umekamatwa asubuhi ya leo, Septemba 9.

Kwa pamoja, mizigo hiyo imehifadhiwa kwenye masanduku 20.

Dkt. Fimbo amesema shehena hiyo ilisafirishwa kutoka Mumbai, India.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa dawa zinazodaiwa kutumika kutibu magonjwa mbalimbali.

Miongoni mwa magonjwa hayo ni saratani, kifua kikuu, kifafa, kisukari na shinikizo la damu.

Mbali na dawa hizo, shehena hiyo pia ilikuwa na vifaa mbalimbali vya tiba.

Vifaa hivyo ni pamoja na meno bandia, zana za upasuaji na glavu.

Dkt. Fimbo amesema baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika na mzigo huo tayari wamekamatwa.

Amesema uchunguzi unaendelea kuwabaini wahusika wengine waliohusika katika usafirishaji na uingizaji wa bidhaa hizo nchini.

Sehemu ya Dawa zisizosajiliwa zilizokamatwa na Tmda.

Ameonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Shehena hiyo nayo itachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.


 Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jiji Dar es salaam.

0/Post a Comment/Comments