DC DODOMA ATOA RAI KWA WANAOISHI KWENYE NJIA ZA MAJI KUHAMA.

......

Na Ester Maile ,Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amewataka wananchi wanaoishi kwenye njia za maji na maeneo hatarishi kuchukua tahadhari mapema, ikiwemo kuhama kwa muda na kuhamisha mali zao, ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua zinazotarajiwa.

Akiizungumza na waandishi Wa habari 18, September 2026 alipotembelea eneo la mradi Wa bwawa la maji linaloendelea kijengwa Katika viwanja vya Nane nane mjini humo,Shekimweri amesema baadhi ya maeneo yaliwahi kukumbwa na mafuriko katika miaka iliyopita, huku maji yakifika hadi magotini, akisisitiza kuwa tahadhari hiyo ni muhimu zaidi kwa familia zenye watoto, wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu ambao wanaweza kupata changamoto wakati wa kuhama.

Amewataka mabalozi wa nyumba kumi, wenyeviti wa mitaa na madiwani kubaini mapema kaya zilizo katika maeneo hatarishi na kuzifikia kwa elimu na tahadhari, huku wananchi wakihimizwa kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo ya viongozi.

Kwa upande wa TANROADS, Meneja wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Filbert Biseko, amesema wameanza kufungua na kusafisha mitaro katika Barabara ya Arusha, pamoja na kuzibua maeneo yenye maji na mchanga katika barabara kuu, huku shughuli za usafi wa mitaro na barabara zikiendelea jijini.

Nao Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wamesema wamejipanga kushirikiana na mamlaka nyingine katika kusafisha mitaro na maeneo yanayoweza kusababisha maji kuziba njia, huku wananchi wakitakiwa kutotumia mitaro kama sehemu ya kutupa taka.

Hatua hizo ni sehemu ya maandalizi ya mamlaka za Dodoma kukabiliana na athari za mvua, huku viongozi wakisisitiza ushirikiano wa wananchi na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha usalama wa watu, mali na miundombinu unalindwa wakati wa mvua.



 

0/Post a Comment/Comments