DEREVA BASI ALIYECHATI AKIENDESHA AKAMATWA MWANZA


.............
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia dereva wa basi la abiria, Sabatho Malima Emmanuel (32), mkazi wa Buswelu wilayani Ilemela, kwa tuhuma za kuendesha gari kwa njia ya hatari huku akitumia simu ya mkononi kuchati.

Dereva huyo alikuwa akiendesha basi la Kampuni ya Obadia lenye namba za usajili T 870 DVW, aina ya Yutong, linalofanya safari kati ya Mwanza na Nyamongo mkoani Mara.

Kwa mujibu wa taarifa, Sabatho alikamatwa Septemba 5, 2026, majira ya saa 6:40 mchana katika eneo la Isangijo wilayani Magu, barabara ya Mwanza–Musoma, akiwa anatokea Nyamongo kuelekea Mwanza.

Inadaiwa kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha basi hilo huku akichati kwa kutumia simu ya mkononi tangu maeneo ya Lamadi mkoani Simiyu, kitendo kilichohatarisha maisha ya abiria waliokuwa ndani ya basi pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa kitendo hicho ni kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani na Usafirishaji, huku hatua za kisheria dhidi yake zikiendelea.
 

0/Post a Comment/Comments