EALA: TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA HUDUMA ZA MATIBABU YA MOYO

........

Na Carlos Claudio, Dar Es Salaam.

Ujumbe wa Kamati ya Mambo ya Jumla ya East African Legislative Assembly (EALA) umeipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika maendeleo ya sayansi ya moyo na mishipa ya damu pamoja na utoaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo.

Kamati hiyo ipo nchini Tanzania kwa ziara maalumu ya siku nne katika Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Moyo na Mishipa ya Damu, ambapo imepata fursa ya kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika elimu, mafunzo, teknolojia na huduma za matibabu ya moyo.

Akizungumza baada ya kutembelea Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mary Mugyenyi, amesema wamevutiwa na maendeleo ya taasisi hiyo pamoja na huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.

Mugyenyi amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujionea matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za afya, kutembelea maabara na kushuhudia namna wagonjwa wanavyopatiwa huduma za matibabu ya moyo.

Amesema maendeleo hayo yanaonesha kuwa nchi za Afrika Mashariki zinaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo ndani ya ukanda huo, hivyo kupunguza ulazima wa wagonjwa kusafiri nje ya bara la Afrika kwa ajili ya kupata matibabu maalumu.

“Leo tumetembelea taasisi ya moyo ambapo tumeona kazi ikifanyika kwa vitendo kwa wagonjwa. Tumeona maendeleo ya teknolojia, tumetembelea maabara na tumefurahishwa sana kuona kwamba huduma za aina hii sasa zinapatikana Afrika Mashariki,” amesema Mugyenyi.

Ameongeza kuwa Kamati hiyo imeona juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuendeleza elimu na mafunzo ya wataalamu wa sayansi ya moyo pamoja na kuimarisha huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye changamoto za moyo.

Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za EALA za kujifunza na kutathmini maendeleo ya huduma na taasisi mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa nchi wanachama.









 

0/Post a Comment/Comments