Na Carlos Claudio, Dodoma
Wajasiriamali katika Wilaya za Bahi na Kondoa mkoani Dodoma, wameeleza kuwa mafunzo ya ujasiriamali na ufugaji wanayopata kupitia mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yamewasaidia kuongeza uelewa na kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
Wajasiriamali hao wameeleza hayo wakati wa zoezi la kugawa vifaranga 2,100 vya kuku chotara kwa wanufaika wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa na INADES Formation Tanzania kwa ufadhili wa Bread for the World.
Wamesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao, hasa kutokana na changamoto ya ukame, huku wakijifunza namna ya kuendesha shughuli za ufugaji kwa tija.
Kwa mujibu wa wanufaika hao, elimu waliyoipata kupitia INADES imewasaidia kuelewa namna bora ya kutunza mifugo, kuongeza uzalishaji na kutumia ufugaji kama njia ya kuongeza kipato na kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Aidha, wameahidi kutumia ujuzi walioupata kuwaelimisha wajasiriamali wengine katika jamii zao ambao bado hawajapata fursa ya kushiriki katika mafunzo hayo.
Mradi huo unalenga kuwasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo yenye ukame kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli za kiuchumi zinazoendana na mazingira yao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Daktari wa Mifugo kutoka INADES Formation Tanzania, Charles Bukula, amesema ugawaji wa vifaranga umefanyika baada ya wanufaika kupata mafunzo ya msingi kuhusu ufugaji bora.
Bukula amesema mafunzo hayo yalilenga kuhakikisha wanufaika wanakuwa na uelewa wa namna ya kutunza kuku, kuzuia magonjwa na kuboresha uzalishaji ili ufugaji huo uweze kuwa chanzo endelevu cha kipato.




Post a Comment