KUMBUKIZI YA MIAKA 121 YA VITA VYA MAJIMAJI YATOA MSUKUMO MPYA KWA URITHI NA UTALII WA KILWA

..........

KILWA MASOKO: Uzinduzi wa Sherehe za Kumbukizi ya Miaka 121 ya Vita vya MajiMaji umefungua fursa na kutoa msukumo mpya katika juhudi za kuhifadhi, kutangaza na kuendeleza urithi wa kihistoria na kiutamaduni wa Kilwa, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kuenzi historia ya mashujaa wa Vita vya MajiMaji.

Sherehe hizo zimezinduliwa leo, Septemba 30, 2026, katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko, na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Malima, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, pamoja na wazee wa mila na viongozi mbalimbali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Malima amesema kumbukizi ya miaka 121 ya Vita vya MajiMaji ni zaidi ya kukumbuka historia, bali ni fursa ya kuitumia historia hiyo katika kujenga kizazi kinachothamini urithi wa Taifa na kuchochea maendeleo kupitia utalii wa kiutamaduni na 

“Ni muhimu kuandikwa kitabu kinachozungumzia  historia ya Vita vya MajiMaji na kuhifadhiwa kwa kuzingatia vyanzo vya wenyeji, simulizi za wazee na maarifa yaliyorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, badala ya kutegemea pekee maandiko yaliyoandikwa na wageni ambao hawakuwa sehemu ya jamii zilizohusika katika historia hiyo, amesema Mhe. Malima

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha maeneo yenye historia ya Vita vya MajiMaji yanatambuliwa, yanahifadhiwa na kutangazwa ili yaweze kunufaisha jamii na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Malima amewataka wananchi, hususan vijana, kuwa sehemu ya juhudi za kulinda na kutangaza urithi wa Kilwa kwa kujifunza historia ya mashujaa wa MajiMaji na kuhakikisha simulizi na maeneo ya kihistoria yanatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amesema kumbukizi hiyo ni fursa muhimu ya kuendelea kuitangaza Kilwa kama eneo lenye utajiri mkubwa wa historia, utamaduni na urithi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika kulinda na kuendeleza urithi huo.

Ushiriki wa wazee wa mila katika uzinduzi huo umeongeza thamani katika jitihada za kuhifadhi maarifa, simulizi na historia zinazorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Aidha, mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kushiriki katika uzinduzi huo umeonesha kuongezeka kwa uelewa na hamasa ya jamii katika kuenzi historia ya mashujaa wa Vita vya MajiMaji na kutambua umuhimu wa urithi wa Kilwa.

Sherehe hizo zinafanyika chini ya kaulimbiu *“MAJIMAJI NA URITHI WA KILWA”,* inayolenga kuunganisha historia ya mapambano ya MajiMaji na urithi mpana wa Kilwa katika kuibua fursa za elimu, utamaduni na utalii.

Kupitia kumbukizi hiyo, Kilwa inapata fursa ya kuendelea kuangazia maeneo yake ya kihistoria na simulizi za mashujaa wa MajiMaji, huku wadau mbalimbali wakihamasishwa kushiriki katika kuyahifadhi, kuyaendeleza na kuyatangaza.

Sherehe za Kumbukizi ya Miaka 121 ya Vita vya MajiMaji zitaendelea na shughuli mbalimbali za kihistoria, kielimu na kiutamaduni, kwa lengo la kuwakutanisha wananchi na wadau katika kuenzi mashujaa wa MajiMaji na kuimarisha uhifadhi wa urithi wa Taifa.

Kumbukizi hiyo inatoa msukumo mpya wa kuhakikisha historia ya Vita vya MajiMaji inaendelea kuwa hai, inafundisha kizazi cha sasa na kijacho, na wakati huo huo inatumika kama nyenzo muhimu katika kukuza utalii wa kihistoria na kiutamaduni wa Kilwa.
















 

0/Post a Comment/Comments