Na Carlos Claudio, Dodoma
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana kikamilifu katika maamuzi na utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikieleza kuwa vijana hawapaswi kuonekana kama kizazi kitakachorithi changamoto hizo pekee, bali pia kuwa sehemu muhimu ya kutengeneza na kutekeleza suluhisho.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa idara ya mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Amina Mbarouk wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Vijana na Watoto kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (LCOY Tanzania), unaofanyika kwa siku tatu hadi Septemba 17, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo, mwakilishi huyo wa Serikali amesema ushiriki wa vijana haupaswi kuishia katika kushauriwa au kusikilizwa, bali wanapaswa kupewa nafasi katika meza za maamuzi, kuibua mawazo na kushiriki katika utekelezaji wa suluhisho za changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi si tishio la mbali tena, bali tayari zinaonekana kupitia mabadiliko ya mifumo ya mvua, ukame, mafuriko, uharibifu wa mifumo ikolojia pamoja na athari katika kilimo na maisha ya wananchi.
“Vijana hawapaswi kuonekana tu kama kizazi kitakachorithi tatizo. Vijana wanapaswa kutambuliwa pia kama kizazi kinachotengeneza na kutekeleza suluhisho,” amesema.
Amesema Serikali inatambua nafasi kubwa ya vijana katika utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi, kutokana na kuwa na nguvu, ubunifu, teknolojia na uwezo wa kuhamasisha jamii.
Mkutano huo umejikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo matumizi ya nishati safi, uhifadhi wa bioanuai na urejeshaji wa mifumo ikolojia, kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, hasara na madhara yatokanayo na tabianchi pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Mwakilishi huyo amesema maeneo hayo hayapaswi kuonekana kama mada za majadiliano pekee, bali ni fursa ambazo vijana wanaweza kuzitumia kubadili changamoto za tabianchi kuwa fursa za maendeleo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, akitaja misitu, ardhi oevu, bahari, wanyamapori na mifumo mingine ya ikolojia kuwa na mchango mkubwa katika kulinda maisha ya wananchi na maendeleo ya taifa.
Amewataka vijana kutumia siku hizo tatu kusikilizana, kushirikiana, kuhoji mifumo iliyopo na kuibua mapendekezo yanayotekelezeka, akisisitiza kuwa tamko litakalotokana na mkutano huo halipaswi kubaki kuwa waraka pekee.
Amesema tamko hilo linapaswa kuwa sauti inayoeleza mahitaji ya vijana, mchango ambao wako tayari kutoa pamoja na matarajio yao kutoka Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wadau wengine.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu za Vijana wa ActionAid Tanzania, Arif Fazel, amesema vijana na watoto wanapaswa kutumia mkutano huo kutoa mawazo na mapendekezo yatakayosaidia Serikali na dunia kwa ujumla kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema maazimio yatakayotokana na mkutano huo yanaweza kuwa na nafasi katika kuathiri msimamo wa Tanzania kuhusu masuala ya tabianchi, kwa kuwa maoni ya vijana yanaweza kuingizwa katika matamko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Fazel amesema athari kama mvua kubwa, mafuriko, upepo mkali, ukame na vimbunga zinaweza kusababisha upotevu wa mali na maisha, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kubadili namna inavyotumia rasilimali ili kupunguza madhara hayo.
Ametoa wito kwa vijana kupendekeza mifumo itakayosaidia kupunguza ukataji miti na matumizi ya mkaa, huku Serikali ikiendelea kuweka njia mbadala za nishati safi na nafuu zinazoweza kumudu wananchi.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya kukabiliana na mafuriko, ikiwemo mifumo bora ya kupitisha maji wakati wa mvua kubwa.
“Msishie kupiga picha, kuchukua namba ya mtu. Sikilizeni mada zilizopangwa, changieni na mchango wenu uwe wa umakini,” amesema.
Naye Mwanzilishi wa Regen Action Tanzania, James Silvester Magesa, amesema vijana na watoto wana nafasi kubwa katika kutafuta na kutekeleza suluhisho za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kuwa sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini.
Amesema mkutano huo unalenga kuwawezesha vijana kujadili changamoto kama ukame na mafuriko na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia kupata suluhisho la changamoto hizo.
“Vijana ni taifa la leo na taifa la kesho. Kwa hiyo tusipowafundisha, sisi ambao tunasemekana ni taifa la kesho lakini sisi ni taifa la leo, mwisho hatutakuwa na wa kumrithisha,” amesema.
Magesa amesema vijana pia wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha hatua za kulinda mazingira.
Amesema takribani vijana 150 wanashiriki mkutano huo, ambao pia unalenga kuandaa tamko litakaloeleza vipaumbele, mahitaji na matarajio ya vijana wa Tanzania kuelekea COP31.
Amesema miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa ni ubunifu na teknolojia mpya, matumizi ya akili bandia (AI), uhifadhi wa mazingira na bioanuai, maji na ardhi pamoja na matumizi ya nature-based solutions katika kukabiliana na changamoto za mazingira na tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Girls Education for Climate Action, Dkt. Happiness Ngonyani, amesema kuwawezesha wanawake, mabinti na vijana kupata elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi ni hatua muhimu katika kuongeza kasi ya kukabiliana na athari zake.
Amesema elimu hiyo itawawezesha wanawake na vijana kushiriki kwa ufanisi zaidi katika kupunguza athari za tabianchi katika jamii.
Naye Katibu wa Regen Action Tanzania, Glory Kaaya, amesema vijana wana ubunifu, ujuzi, vipaji na mawazo ambayo yakipewa nafasi yanaweza kusaidia kutatua changamoto za mazingira na tabianchi.









Post a Comment