Na Sixmund Begashe, Moshi
Wachezaji wa Maliasili Sports Club wamepongezwa kwa juhudi na kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mashindano ya SHIMIWI 2026, yanayoendelea mkoani Kilimanjaro.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Bw. Bernard Marcelline, alipokutana na wanamichezo wa Maliasili Sports Club katika viwanja vya Chuo cha Polisi (CCP), vilivyopo mkoani humo.
Bw. Marcelline amesema amejionea namna timu zinazoiwakilisha Wizara ya Maliasili na Utalii zinavyojituma kwa hali na mali katika michezo mbalimbali, jambo ambalo, kwa mujibu wake, linaonesha wazi kuwa timu hizo zina nafasi nzuri ya kuendelea kupata ushindi katika michezo inayofuata.
Kauli hiyo ameitoa baada ya timu ya wanawake ya Kamba kufanikiwa kutinga hatua ya 18 bora katika mashindano hayo, huku akiwataka wanamichezo kuongeza juhudi na kujituma zaidi ili kufikia malengo yaliyowekwa.
“Maliasili, ushindi upo wazi. Tuna uhakika katika mashindano haya tutaibuka washindi na kurudi Wizarani na vikombe vya kutosha,” amesema Bw. Marcelline.
Pamoja na hayo, Marcelline amesisitiza kuwa juhudi na mshikamano miongoni mwa wanamichezo hao ni muhimu katika kuhakikisha timu hizo zinaendelea kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Aidha, amewataka wanamichezo hao kutumia michezo hiyo kama fursa ya kuonesha uwezo wao, huku wakizingatia maelekezo wanayopewa na viongozi na makocha wao ili kuongeza uwezekano wa kupata ushindi katika michezo inayofuata.
Bw. Marcelline amewahakikishia wanamichezo hao kuwa uongozi wa Wizara upo bega kwa bega na Maliasili Sports Club, na kwamba unaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wanamichezo hao katika mashindano hayo yanayoendelea Moshi, Kilimanjaro, mwaka 2026.
Akizungumza kwa niaba ya wanamichezo hao, Mwenyekiti wa Maliasili Sports Club, Bw. Elia Mtalemwa, ametumia hiyo kuushukuru uongozi wa Wizara kwa ushirikiano unaooneshwa kwa wanamichezo hao, kuanzia katika maandalizi ya mashindano hayo hadi sasa.






Post a Comment