MKURUGENZI WA FDH ATOA WITO WA KULINDA AMANI

.....

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani nchini, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo na usalama wa makundi yote katika jamii, wakiwemo watu wenye ulemavu.

Salali ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa semina iliyolenga kuwajenga viongozi wa Tanzania Peace Familykupitia mafunzo kuhusu amani na uzalendo, ili kuwawezesha kuwa mabalozi wa amani watakaohamasisha na kutetea amani wanapokuwa katika maeneo mbalimbali.

Amesema FDH, ambalo limekuwa likifanya kazi ya kutetea na kusaidia makundi ya watu wenye ulemavu, linajisikia faraja kushirikiana na Tanzania Peace Family katika juhudi za kuimarisha amani nchini.

“FDH iko tayari kushirikiana na Tanzania Peace Family na tuko tayari kutoa rasilimali, nguvu na maarifa kuhakikisha tunashirikiana pamoja kuilinda amani yetu,” amesema Salali.

Ameeleza kuwa uwepo wa taasisi zinazohamasisha amani ni muhimu kwa watu wenye ulemavu, kwani amani inapokosekana, makundi hayo yanaweza kuwa miongoni mwa wanaoathirika zaidi.

Salali amewataka viongozi wa Tanzania Peace Family kutokuchoka katika kuhamasisha amani, akisisitiza kuwa Tanzania inahitaji amani ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za maendeleo kwa usalama.

Aidha, amesema vijana wanahitaji kuendelea kujifunza kutoka kwa viongozi na watu wenye uzoefu ili waweze kuelewa umuhimu wa kulinda amani na kuhakikisha vizazi vijavyo vinaendelea kuishi katika mazingira salama.

Sambamba na hayo amewahimiza watanzania wote kujumuika pamoja katika ulinzi wa amani lakini piq kuendelea kuliombea taifa ili kuweza kudumisha amani na mshikamano wa pamoja

Kwa upande wake, Mratibu Taifa wa Tanzania Peace Family, Matrona Remigeus Severine, amesema taasisi hiyo imejikita katika kushiriki katika utatuzi wa migogoro ya kidini, kisiasa na kijamii kwa ujumla.

Amesema kabla ya viongozi wa taasisi hiyo kwenda kwa wananchi kueneza ujumbe wa amani, wanapaswa kwanza kujengwa katika misingi ya uzalendo, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Severine amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuwajengea viongozi uwezo wa kuwa mabalozi wa amani na uzalendo katika jamii, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika kulinda amani ya Tanzania.
 

0/Post a Comment/Comments