NEMC YATOA WITO KWA WANANCHI KUTUNZA USAFI WA VITUO VYA MABASI

............

DAR ES SALAAM — Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, NEMC, limewataka wananchi kuacha kutupa taka hovyo katika vituo vya mabasi na maeneo mengine ya umma.

Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini wa NEMC, Bi. Glory Kombe, amesema wananchi wanapaswa kutumia vyombo vya taka vilivyowekwa katika maeneo hayo.

“Kila mmoja awajibike, tusitupe taka hovyo.”

Amesema wafanyabiashara, hasa wanaouza maji, pipi na biskuti, wanapaswa kukusanya taka zinazotokana na biashara zao na kuziweka katika sehemu sahihi.

Wito huo umetolewa kuelekea Tamasha la Michezo na Mazingira litakalofanyika kesho, tarehe 25 Septemba, Kata ya Bunju A, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuhusu usafi na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Balozi wa Mazingira wa Kujitolea kwa Jamii, Moses Mwakibolwa, amesema wananchi hawapaswi kuacha jukumu la usafi kwa wakandarasi pekee.

“Usafi si wa mkandarasi pekee; ni jukumu la kila mwananchi.”

Mwakibolwa amesema hatua ndogo za wananchi, ikiwemo kuokota taka na kuzitupa katika maeneo sahihi, zinaweza kusaidia kujenga mazingira safi.

Tamasha hilo pia linalenga kuhamasisha dhana ya Taka Zero, kwa wananchi kutenganisha na kutumia taka kama fursa badala ya kuzitupa ovyo.

Taka Zero inaanzia kwako.

 

0/Post a Comment/Comments