PSPTB YATOA SIKU 30 KWA WATAALAMU WENYE MADENI YA ADA

...........

Na Carlos Claudio, Dodoma

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imewataka wataalamu wote waliosajiliwa ambao bado wana madeni ya ada za mwaka kulipa madeni hayo yote ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa tangazo hilo, vinginevyo usajili wao utafutwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisema wataalamu watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watakabiliwa na hatua mbalimbali kwa mujibu wa sheria.

Amesema hatua hizo ni pamoja na kufutwa mara moja kwa usajili, huku majina ya watakaokaidi yakitarajiwa kuchapishwa rasmi kwenye tovuti ya PSPTB na Gazeti la Serikali.

Mbanyi amesema pia hatua zaidi za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wataalamu hao, ikiwemo kufunguliwa mashitaka kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha PSPTB.

Ameeleza kuwa PSPTB ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB, Sura ya 179 ya Sheria za Tanzania, ikiwa na jukumu la kusimamia na kudhibiti viwango, mwenendo na maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Kifungu cha 7(g) cha Sheria ya PSPTB kinaipa Bodi mamlaka ya kipekee ya kusajili watu wanaokidhi vigezo na kuwapa mamlaka ya kisheria ya kufanya kazi kama wataalamu wa ununuzi na ugavi.

Amesisitiza kuwa mtu ambaye hajasajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria hiyo hana uhalali wa kushiriki au kufanya kazi za ununuzi na ugavi.

Aidha, amesema kwa mujibu wa Kanuni za PSPTB, Tangazo la Serikali Na. 364 la mwaka 2009, pamoja na masharti mengine ya sheria hiyo, kila mtaalamu aliyesajiliwa ana wajibu wa kisheria kulipa ada ya mwaka kwa wakati, kama inavyowekwa na Bodi.

Mbanyi amesema mtaalamu yeyote anayeshindwa kulipa ada kwa kipindi cha miezi 24 mfululizo atachukuliwa kuwa amepoteza hadhi yake ya usajili na jina lake linaweza kuondolewa kwenye daftari rasmi la usajili la PSPTB.

Amesema Bodi haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayeendelea kufanya kazi au kujitambulisha kama mtaalamu wa ununuzi na ugavi bila kuwa na usajili halali.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 46(2) na (3) cha Sheria ya PSPTB, amesema mtu anayeendelea kujihusisha na taaluma hiyo bila kusajiliwa anafanya kosa la jinai na anastahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Ameongeza kuwa hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa pia kwa kuzingatia Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Tangazo la Serikali Na. 365 la mwaka 2009 (PSPTB Code of Ethics and Conducts).

PSPTB imesisitiza kwa wataalamu wote wenye madeni ya ada kuchukua hatua za haraka kulipa madeni yao ndani ya muda uliowekwa ili kuepuka kupoteza usajili wao na kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.



 

0/Post a Comment/Comments