Na Carlos Claudio, Dodoma.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali itaendelea kuboresha mchakato wa udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu nchini kwa lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata elimu ya juu bila kuathiri ubora wa elimu.
Prof. Mkenda ameyasema hayo Septemba 5, 2026, jijini Dodoma, baada ya kukutana na Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu pamoja na Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu nchini, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu elimu ya juu, hususan mchakato wa udahili na usajili wa wanafunzi.
Amesema wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu wanapaswa kuendelea na maombi yao, huku akieleza kuwa Serikali itatoa utaratibu zaidi utakaowawezesha wanafunzi na vyuo kufuata mchakato huo kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imeweka utaratibu unaolenga kulinda maslahi ya vyuo pamoja na wanafunzi, huku ikisisitiza umuhimu wa vyuo kutosajili wanafunzi zaidi ya uwezo wao wa kutoa mafunzo.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu haliathiri ubora wa elimu inayotolewa nchini.
“Tunataka kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata elimu ya juu, lakini hatutaki kufanya hivyo kwa kushusha ubora wa elimu,” amesema.
Prof. Mkenda amesema Serikali pia imeendelea kuwekeza katika kuongeza uwezo wa vyuo vikuu nchini, ikiwemo ujenzi wa kampasi katika mikoa mbalimbali, hatua ambayo itaongeza nafasi za udahili na kusaidia kuongeza kiwango cha uandikishaji wa elimu ya juu.
Aidha, amesema Serikali itakutana na viongozi wa vyuo vya kati vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa ajili ya kujadili masuala ya ubora wa elimu, usajili pamoja na usimamizi wa udahili.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, amesema suala la ubora wa elimu ni endelevu na linahitaji ushirikiano wa Serikali, TCU na vyuo vikuu ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Prof. Alfred Sife, amesema kikao hicho kimejadili namna bora ya kuboresha mchakato wa udahili ili vyuo viweze kupata wanafunzi wenye sifa na uwezo unaohitajika katika masomo ya elimu ya juu.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Teknolojia na Biashara (TEKU), Dkt. Aggrey Mlimuka, amesisitiza umuhimu wa vyuo kuendelea kusimamia viwango vya ubora wa elimu ili kuhakikisha vinazalisha wataalamu wenye weledi na uwezo katika taaluma mbalimbali.





Post a Comment