SERIKALI YACHUKUA HATUA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU WILAYANI ITILIMA

...........

Na Mwandishi Wetu, Simiyu 

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo wanaovamia maeneo ya makazi na mashamba ili kuokoa maisha ya wananchi na mali zao.

Mhe. Chande amesema hayo Wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) ya kusikiliza kero na kutatua changamoto kwa wananchi wa maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mhe. Chande amebainisha hatua hizo kuwa ni pamoja na matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone), kufunga visukuma mawimbi kwa makundi ya tembo zaidi ya nane kwa lengo la kubaini mwenendo na mwelekeo wa makundi hayo, kuongeza idadi ya askari na kujenga vituo viwili vya askari wa wanyamapori katika maeneo ya vijiji kwa ajili ya mwitikio wa haraka wa kuwadhibiti kabla hawajasababisha madhara kwa binadamu na mali zao.

Aidha, amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo tembo sambamba na kuanzisha vikundi vitatu venye watu 52 kwa ajili ya kushirikiana na wahifadhi kukabiliana na changamoto hiyo.

Vilevile, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kushughulikia madai ya kifuta jasho na kifuta machozi kutoka kwa wananchi wa Itilima ambao waliathiriwa na wanyamapori hao kwa namna moja ama nyingine ambapo amesema kuwa tayari baadhi ya madai hayo yameanza kulipwa na mengine yakiwa katika hatua mbalimbali za malipo.












 

0/Post a Comment/Comments