SERIKALI YAWEKEZA SH. BILIONI 698 KUKAMILISHA MJI WA SERIKALI MTUMBA

......

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Serikali imesema imewekeza jumla ya Sh. bilioni 698 hadi sasa katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukamilisha uhamishaji wa shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema hayo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa majengo ya Wizara, Taasisi za Serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, unaotarajiwa kufanyika Septemba 8, 2026.


Uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atakuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, Mji wa Serikali Mtumba.


Prof. Kabudi amesema uzinduzi huo utahusisha majengo ya Ofisi za Wizara 26, Taasisi za Serikali 11 pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1, hatua anayosema ni muhimu katika kuimarisha hadhi ya Dodoma kama kitovu cha shughuli za Serikali.


Amesema kukamilika kwa majengo hayo kutaiwezesha jumla ya watumishi 18,510 kufanya kazi katika Ofisi za Mji wa Serikali Mtumba, hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji wa Serikali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, ujenzi wa Mji wa Serikali ulianza kutekelezwa kwa awamu, ambapo Awamu ya Kwanzailihusisha ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za muda ulioanza Novemba 28, 2018 na kukamilika Machi 22, 2019.


Majengo hayo ya awali yaliwezesha baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali kuhamia Mtumba, sambamba na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na jengo la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).


Amesema Awamu ya Pili, iliyoanza Oktoba 2021, imehusisha ujenzi wa majengo ya kudumu kwa ajili ya Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na miundombinu muhimu ya kudumu.


Miundombinu hiyo inajumuisha barabara za lami kilomita 57.1, mifumo ya mawasiliano, Uwanja wa Mashujaa na huduma nyingine za kijamii. Aidha, Serikali inaendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42, mifumo ya maji safi na maji taka, TEHAMA, mifumo ya usalama ya CCTV, kituo cha zimamoto pamoja na mpango wa upandaji miti na uendelezaji wa mandhari ya Mji wa Serikali.


Prof. Kabudi amesema utekelezaji wa mradi huo umehusisha kwa kiasi kikubwa wakandarasi na watoa huduma wa ndani, hatua inayolenga pia kuchochea matumizi ya utaalamu na uwezo wa ndani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa.


Amesema ujenzi wa majengo ya Wizara na Taasisi katika Awamu ya Pili unatekelezwa na wakandarasi 11, ambapo watano ni taasisi za Serikali na sita ni kampuni kutoka sekta binafsi.


Aidha, washauri elekezi watano wanaosimamia utekelezaji wa kazi hizo wote ni taasisi za Serikali, zikiwemo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kampuni ya Ushauri ya Chuo Kikuu Ardhi (ABECC), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Watumishi Housing Investment.


Kwa upande wa miundombinu, Serikali imeshirikisha taasisi mbalimbali ikiwemo TARURA kwa ujenzi wa barabara, DUWASA kwa mifumo ya maji safi na maji taka, TANESCO kwa miundombinu ya umeme, TTCL kwa mifumo ya mawasiliano na TEMESA kwa usimikaji wa mifumo ya CCTV.


Taasisi nyingine zinazoshiriki ni Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).


Waziri huyo amesema ubunifu wa majengo na miundombinu ya kudumu katika Awamu ya Pili umezingatia dhana ya “Mji Janja” (Smart City), ikiwemo ujenzi wa mji wa kijani, matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, uzingatiaji wa sheria za mipango miji, Mpango Kabambe wa Mji wa Serikali na tathmini ya athari kwa mazingira.


Majengo hayo yamegawanyika katika miundo minne kulingana na mahitaji ya taasisi na idadi ya watumishi. 


Baadhi yana uwezo wa kuchukua watumishi 300, mengine 500, majengo makubwa yana uwezo wa kuchukua hadi watumishi 1,400, huku majengo ya taasisi yakiwa na uwezo wa kuchukua takribani watumishi 150.


Prof. Kabudi amesema Serikali pia imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, ambapo Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani za Wizara na Taasisi 26 zitakazohamia katika majengo hayo.


Amesema uwekezaji huo unaifanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa zaidi ya eneo la ofisi, bali kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali, huku ukifungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.


Akizungumzia barabara zilizojengwa, Prof. Kabudi amesema miundombinu hiyo itarahisisha usafiri ndani na nje ya Mji wa Serikali, kuboresha mawasiliano na kurahisisha wananchi kufika katika Ofisi za Serikali na maeneo mbalimbali bila usumbufu.

“Mji wa Serikali Mtumba ni zaidi ya majengo. Ni uwekezaji katika ufanisi wa Serikali, ni uwekezaji katika Dodoma, na ni sehemu ya safari ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara, huduma bora na miundombinu ya kisasa,” amesema.



 

0/Post a Comment/Comments