..........
Na Daniel Limbe
"SAMAKI mkunje angali mbichi" ndivyo wasemavyo wahenga wakimaanisha ni rahisi sana kumfundisha mtu au kumlea mtoto katika maadili na tabia njema akiwa bado mdogo kuliko kongoja hadi akue na kukomaa.
Msemo huo unaakisi wazi kuwa Mzazi, mlezi au jamii inayonafasi kubwa ya kuandaa kizazi bora au kibaya kutokana na kuwapandikizia watoto mambo mbalimbali ambayo hujenga aina ya maisha ya kesho yao.
Maneno hayo yanauweka bayana ukweli wa maisha ya mwanadamu katika malezi na makuzi ya mtoto hata anapokuwa mtu mzima.
Ukweli huo unaungwa mkono na kitabu kitakatifu cha Biblia katika Mithali 22:6 ambayo inasema "Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapo kuwa Mzee.
Kwa lugha nyepesi ni kwamba matendo yasiyofaa kwa jamii ikiwemo ukatili, mauaji, uchoyo, ufisadi, husda, dhuruma, na mengineyo mengi kwa kiwango kikubwa yanachangiwa na malezi na makuzi mabovu kutoka kwa wazazi au walezi.
Kutokana na ukweli huo, baadhi ya taasisi binafsi za elimu zimelazimika kurejea katika mafundisho mema ya kuwaandaa watoto katika maadili mema ili kujenga kizazi bora kwa maisha ya leo na kesho iliyonjema.
Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Shule za awali, msingi na sekondari za Victory zilizopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera ambapo katika viwanja vyake ya shule ya msingi kuligeuka shamrashamra, shangwe na nderemo baada ya wazazi na walezi kushuhudia vipaji vikubwa vya watoto wao walio waliohitimu elimu ya darasa la Saba mwaka 2026.
Mbali na mafanikio ya ufaulu wa kitaaluma kwa shule hizo, shangwe na furaha viliongezeka zaidi baada ya wanafunzi wa shule ya msingi Victory kuonyesha uwezo wao mkubwa wa kuzungumza lugha ya Kichina.
Pia wazazi walishuhudia wahitimu 50 wakiwa na uwezo mkubwa wa masomo ya sayansi na teknolojia huku somo la maadili mema likitajwa kama siri kubwa ya mafanikio ya shule hizo.
Makamu Askofu wa Kanisa la "The Evangelistic Assemblies of God in Tanzania" (EAGT) Kanda ya Kagera, Hosea Sentozi ni miongoni mwa wageni muhimu waliohudhuria mahafali ya tisa ya shule hiyo, ambapo mbali na mambo mengine ameonekana kufurahishwa zaidi ya maadili mema yanatolewa na walimu wa shule hiyo ambapo suala la malezi ya kimwili na kiakili wamelipa kipaumbele kikubwa.
Anasema alichokishuhudia hapo kinaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa jamii kutokana na kuwa na viongozi wazuri wenye maadili na hofu kubwa ya Mungu.
Askofu Sentozi anaisisitiza jamii kutoogopa kuwekeza kwenye elimu kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuweza kulivusha taifa lolote duniani iwapo litakuwa limedhamiria kusonga mbele ki elimu , kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.
Anaupongeza uongozi wa shule hizo kwa kutambua thamani ya kuwafundisha watoto lugha za kimataifa ikiwemo Kichina na kwamba itasaidia kuwa na vijana wenye uelewa mpana wa elimu na lugha za kimataifa hali itakayoongeza ushindani katika soko la ajira la ulimwengu pamoja na nchi wanachama wa Afrika mashariki (EAC).
Kauli ya Askofu Sentozi, inaungwa mkono na tungo ya mwanamuziki wa Kitanzania Banza Stone inayosema "Ikiwa unaona elimu ni ghari basi jaribu ujinga".
Kumbe alimu ni bora zaidi kuliko ujinga kama asemavyo Mwanafalsafa Eleanor Roosevelt kuwa " Elimu kubwa hujadili mawazo, akili ya wastani hujadili matukio, na akili ndogo huzungumzia watu "(majungu).
NGUZO YA MAFANIKIO YA SHULE ZA VICTORY
Mkurugenzi wa shule za Victory, Paulo Sentozi, anasema mafanikio ya shule hizo yanatokana na utashi wa ki Mungu kuamua kusaidia jamii katika nyanja ya elimu ili kuwa na jamii yenye maarifa na utambuzi wa jema na baya.
Chini ya usimamizi thabiti wa serikali kwa kushirikiana na walimu, wazazi na Bodi ya shule hiyo umekuwa mhimili wa kuendelea kufanya vizuri sana ki elimu ndani ya wilaya ya Biharamulo, mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla, hali iliyosababisha kutunukiwa tuzo mbalimbali ikiwemo ya shule ya kwanza kitaifa kwa somo la Uraia na maadili mwaka 2021.
Wakati shule hiyo ikisherehekea mahafali ya tisa tangu kuanzishwa kwake, kumbukumbu zinaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi 320 wamehitimu hapo na kuendelea na masomo ya elimu ya juu na vyuo vya kati kwa mafanikio makubwa.
Paulo anasema kutokana na kutambua kuwa msingi bora wa mwanadamu unaanzia chini, shule hiyo pia imekuwa ikihakikisha watoto wote wanaosoma katika shule za Victory wanaondoka na ufaulu mzuri pamoja na maadili mema, kitu ambacho kimekuwa kivutio kikubwa kwa wazazi na walezi kutoka sehemu mbalimbali nchini kupeleka watoto wao katika shule hizo.
"Ndiyo maana tumeamua kupambana sana katika suala zima la elimu kwa watoto wetu, kwa kutambua kuwa ili uweze kuwa na jamii bora na iliyostaarabika lazima uwe na vijana wenye maarifa, ustadi na ubunifu wa hali ya juu katika Tehama kwa kuwa Dunia inabadilika"
"Tunachokishuhudia sasa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa katika upanuzi wa shule zetu ili kuimarisha utoaji wa taaluma bora zaidi na tunaahidi kuendelea kujiimarisha zaidi si kwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza pekee, bali kwa wahitimu wetu kuondoka wakiwa na ujuzi mkubwa utakao kuwa msaada kwao na jamii kwa ujumla" amesema Paulo.
Kauli ya Mkurugenzi huyo inakwenda sambamba na alichowahi kusema Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela kuwa "Elimu ni silaha yenye nguvu, yenye uwezo wa kuibadilisha Dunia".
Ili kuendelea na mpango mkakati wa elimu kwa vitendo, pia wamelazimika kuwekeza elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ikiwa ni njia muafaka kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata kilicho bora zaidi.
Hata hivyo, Paulo ameendelea kusisitiza jamii kutambua thamani ya uwekezaji wa maisha ya elimu kwa watoto wao na kwamba kamwe hawatojuta kupeleka wanafunzi katika shule za Victory kutokana na nia njema ya kuinua taaluma nchini.
WAZAZI WATOA NENO
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma kwenye shule za Victory wameelezea matarajio ya watoto wao, akiwemo Joviness Kasian, ambaye ni Mkazi wa Biharamulo anasema kuwa shule hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo na mkoa wa Kagera kwa ujumla.
Anasema elimu ni gharama licha ya kuwa shule hizo zimekuwa na punguzo kubwa la ada na baadhi ya wazazi kulipa pesa kwa awamu tofauti ili kuhakikisha watoto wao hawakwami kuendelea na masomo.
Akizungumzia kuhusu taaluma anasema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri sana hata katika matokeo ya mitihani ya ndani na nje ya wilaya, mkoa na ile ya kitaifa.
Hatua hiyo imekuwa ikiwasukuma wazazi wengi kupeleka watoto wao katika shule hizo kwa kuwa zinafanya vizuri katika ufundishaji pamoja na kusimamia maadili ya watoto ikiwemo kuheshimiana, kuheshimu wakubwa na wadogo pamoja na walezi.
Vile vile shule hiyo imekuwa ikifundisha Tehama hatua inayowaandaa watoto kuwa na ujuzi hata baada ya kuhitimu katika shule hizo.
"Shule hii ya msingi Victory tunaipongeza na kuwashukuru sana viongozi wake kwa kuwa makini sana katika ufundishaji pamoja na miundo mbinu yake, ispokuwa tunaomba wajitahidi pia kuongeza ukubwa wa ukumbi wa shule ili wazazi tunapokuja kwenye mahafali ya watoto wetu wote tuwe tunapata nafasi za kukaa ndani" amesema Fikiri Misana.
MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO
Hakuna ubishi kwamba suala la elimu bora ni muhimu liende sambamba na malezi na makuzi ya mtoto.
Ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto wetu wanapata malezi na makuzi bora yatakayo waandaa kuwa viongozi na watumishi wema katika taifa letu badala ya kuwa na viongozi wenye wivu, husda, wizi, majungu, ufisadi, majambazi na wenye roho za korosho.
Kwa msingi huo, malezi bora hutengeneza kesho njema ya mtoto, huwaandaa kifikra na kitabia, maisha ya mtoto wako na msingi uliompa leo ndiyo utakaomwezesha kuwa na maisha ya Baba na mama bora ajaye.
Na kama kweli tunataka kujenga taifa imara lenye weledi, umahiri na uwezo wa kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa, basi ni lazima tuwekeze kwa watoto pasipo kutazama gharama.
Dunia ya kesho haitatudai pesa, barabara, bandari wala magari itatudai mbegu ya maadili na elimu bora inayoendana na wakati uliopo.
Malezi ni shule ambayo tunaweza kuitumia kupandikiza roho ya ukweli, upendo kati ya mtu na mtu, kati ya familia na familia, taifa na taifa na kati ya bara na bara jingine.
Ni muhimu tuzibe ufa kabla ya kujenga ukuta kwa kuhakikisha kila mzazi au mlezi, serikali, jamii na wadau wengine waaendeleo tuwe tayari kuwa daraja la elimu na malezi bora kwa watoto wetu.
Dunia ya sasa inalilia amani, kutokana na kupotea kwa maadili na malezi bora,tunaishi katika ulimwengu ambao kwa nyakati tofauti hauna huruma kabisa na wakati mwingine tunatamani kuishi bila Mungu.
UTAFITI
Katika utafiti wa Daktari wa Magonjwa ya akili nchini Uingereza, John Bowlby, ulioitwa "Meternal Deprivation Hypothesis" ulionyesha kuwa iwapo uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto utavunjwa, upo uwezekano mkubwa wa kuathirika maendeleo ya mtoto kihisia, kiakili na kisaikolojia.
Pia ukosefu wa uhusiano mwema kati ya wazazi na mtoto ni zao la kile alichokiita kutokuwa na huruma kwa watu wengine (Affectionless Psychopathy).
Aidha uwepo wa wauaji wa mfululizo, waharifu, magaidi, jeuri, na madikteta kuna uhusiano wa karibu wa tatizo la kiwewe, ukatili, kutelekezwa, pamoja na kukosa ukaribu wa kihisia katika malezi na makuzi yao wakati wa utoto.
Hata hivyo, wengine hukumbwa na tabia hizo kutokana na kufiwa na wazazi wao, ulevi wa kupindukia wa wazazi wao, uraibu wa dawa za kulevya pamoja na ugonjwa wa akili.
Utafiti mwingine uligundua kuwa aslimia 50 ya wauaji wa mfululizo walinyanyaswa kisaikolojia wakati wa utotoni, huku aslimia 36 ikionyesha walinyanyaswa kimwili na aslimia 26 walinyanyaswa kingono.
Katika historia ya wauaji wa mfululizo kama vile David Berkowitz, Ted Bundy na Joel Rifkin walikataliwa au kuachwa na mama zao.
Muuaji Edmund Kemper katika malezi yake yeye aliteswa na kunyanyaswa kisaikolojia na mama yake mzazi.
Vile vile muuaji wa kike Aileen Wuornos aliyeonyeshwa na Charlize Theron katika filamu ya Monster, aliachwa na mama yake akiwa na umri wa miaka minne tu na kulelewa na Babu yake, ambaye alimnyanyasa kimwili na kingono.
Baba yake Aldof Hitler, alikuwa mlevi na mwenye jeuri, huku mama yake akiwa amehudhunishwa na kupoteza watoto watatu wa awali, hivyo hakuweza kumpa uangalizi na upendo.
Benito Mussolini na Francisco Franco walikuwa watoto wa Baba walevi na jeuri, ambapo wakingali wadogo, Mussolini na Franco wote walionyesha uwepo wa dalili za ukatili wa kisaikolojia na kutojali Kabisa hisia za wengine.
Kingali akiwa mdogo, Mussolini alikuwa jambazi mwenye jeuri ambaye alifukuzwa shuleni kwa kumchoma kisu mwanafunzi mwenzake.
Kadhalika Baba yake Saddam Hussein na Kaka yake mkubwa wote walikufa muda mfupi kabla ya kuzaliwa kwake, na kumwacha mama yake akiwa na kiwewe kiasi cha kwamba alimkataa Saddam, kisha akachukuliwa mjomba wake.
Saddam Hussein akiwa mtoto pekee wa mama asiye na mwenza, alionewa kila mara na kupigwa akiwa mtoto na alijifunza jeuri ili kujitetea.
Vyema itambulike kuwa mtoto asipopewa malezi bora yenye huruma na mapenzi mema katika umri wa miaka yake ya mapema tangu kuzaliwa kwake, upo uwezekano mkubwa wa kuharibu uwezo wake wa huruma.




Post a Comment