*******
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza kuchukua tahadhari kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kueleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuimarika katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi Oktoba mwaka huu.
Hayo yameelezwa wakati Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chan’ga aliipokutana na menejimenti, wafanyakazi na wataalamu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu hali ya El Niño na namna ya kutumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magara, amesema shirika hilo limechukua tahadhari kubwa kutokana na ukweli kwamba shughuli zake nyingi za uchimbaji, utafiti na uchenjuaji wa madini hufanyika katika maeneo ya porini ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua kubwa.
Amesema mvua nyingi zinaweza kusababisha usumbufu katika shughuli za uchimbaji na shughuli nyingine zinazohusiana na madini, hali ambayo inaweza kuathiri uzalishaji na mapato ya STAMICO.
Amesema mapato makubwa ya shirika yanatokana na shughuli zinazofanyika katika maeneo hayo, hivyo kuvurugika kwa operesheni kutokana na mvua kunaweza kuathiri pia mapato ya STAMICO.
Ameongeza kuwa STAMICO itaendelea kuwaelimisha watumishi wake waliotawanyika katika maeneo mbalimbali nchini na kuhakikisha wanafuatilia taarifa na maelekezo yatakayotolewa na TMA.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Chan’ga, amesema hali ya El Niño ipo na kwamba mamlaka hiyo inatarajia mvua kuanza kuimarika katika maeneo mbalimbali ya Tanzania katika kipindi cha mwisho wa Septemba na mwanzoni mwa Oktoba.
Amesema kuanzia wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba, mvua zinatarajiwa kuanza kuimarika katika ukanda wa Ziwa Victoria, hususan mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.








Post a Comment