STAMICO YAIBUKA NA RAFIKI BRIQUETTES, UWT WACHANGAMKIA FURSA YA NISHATI SAFI

.....

Na Carlos Claudio, Dodoma

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini kupitia bidhaa yake ya Rafiki Briquettes, huku wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wakionesha shauku ya kutumia na kusambaza nishati hiyo.


STAMICO imeendesha mafunzo kwa wajumbe wa Baraza Kuu la UWT pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa UWT kutoka wilaya mbalimbali nchini, katika ukumbi wa White House jijini Dodoma, Septemba 22, 2026.


Akitoa mafunzo hayo, Meneja wa Masoko na Mahusiano ya Umma wa STAMICO, Deus Alex Ntukamazina, ameeleza kuwa Rafiki Briquettes zina uwezo wa kuwaka kwa muda mrefu na zinaweza kutumika katika shughuli mbalimbali za nyumbani, ikiwemo kupikia, kuchoma nyama na kuchemsha vitu mbalimbali.


Amesema pia nishati hiyo inaweza kutumika viwandani kwa shughuli kama kukausha mazao na kuzalisha joto kwa ajili ya michakato mbalimbali ya uzalishaji.


Aidha, Ntukamazina ameeleza kuwa Rafiki Briquettes zinatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo kuwa mawakala na wasambazaji wa nishati hiyo na hivyo kujipatia kipato.


Amesema bidhaa hiyo imepata uthibitisho kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na STAMICO inatumia teknolojia maalumu ya carbonizer inayosaidia kupunguza joto la briquettes, kulinda vyombo vya kupikia pamoja na kupunguza hewa ukaa na hewa nyingine zinazoweza kuwa na madhara kwa afya.


Kwa upande wao, wajumbe wa UWT walionesha kuvutiwa na nishati hiyo na kuiomba STAMICO kuendelea kutoa mafunzo katika maeneo mbalimbali nchini. Wengine walionesha nia ya kuwa mawakala wa Rafiki Briquettes na kuahidi kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi kama mbadala wa kuni na mkaa.




Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mhe. Mary Chatanda (MCC), amewataka wajumbe kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa wasambazaji wa Rafiki Briquettes katika maeneo mbalimbali nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza matumizi ya nishati safi.


STAMICO imesema itaendelea kusambaza kwa kasi Rafiki Briquettes ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama, kwa lengo la kulinda mazingira na afya za Watanzania.







0/Post a Comment/Comments