Serikali imetakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuweka mifumo bora ya usimamizi wa taka za masokoni ili kuzigeuza kuwa fursa za kiuchumi, ajira na kipato kwa wananchi.
Wito huo umetolewa wakati wa warsha ya uhamasishaji na kujenga uwezo kuhusu mpango wa “Market Waste to Wealth”, iliyofanyika Mbezi, jijini Dar es Salaam, ikilenga kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya taka kama rasilimali.
Washiriki wameelezwa kuwa taka za kikaboni zinazotokana na masoko zinaweza kuchakatwa na kuzalisha bidhaa zenye thamani, ikiwamo mbolea ya mboji na chakula cha mifugo kwa kutumia teknolojia ya Black Soldier Fly Larvae (BSFL).
Aidha, imesisitizwa kuwa utenganishaji wa taka kwenye chanzo ni muhimu kwa kurahisisha ukusanyaji, usafirishaji na uchakataji wa taka hizo ili ziweze kuleta manufaa ya kiuchumi.
Warsha hiyo imeeleza kuwa usimamizi wa taka si jukumu la Serikali pekee, bali unahitaji ushiriki wa wafanyabiashara, Serikali za Mitaa, sekta binafsi, taasisi za fedha, mashirika na wadau wa mazingira.
Katika hatua hiyo, wanawake na vijana wametajwa kuwa na nafasi kubwa katika uchumi wa mzunguko, kutokana na ushiriki wao katika biashara za masoko pamoja na uwezo wao katika ubunifu, teknolojia na ujasiriamali.
Aidha, imeelezwa kuwa usimamizi bora wa taka una mchango mkubwa katika kulinda afya ya jamii kwa kupunguza uchafuzi wa mazingira, harufu, wadudu, magonjwa na taka zinazopelekwa dampo.
Warsha hiyo imehitimishwa kwa wito wa kuendeleza ushirikiano kati ya GEHESE, Manispaa ya Ubungo, wafanyabiashara na wadau wengine ili kujenga masoko safi, salama na yenye kutumia taka kama rasilimali ya maendeleo endelevu.

Post a Comment