........
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimesema hakina mgogoro wala ugomvi na Serikali, bali kinaendelea kushirikiana nayo kwa karibu katika kuhakikisha haki na maslahi ya wafanyakazi yanapatikana kwa wakati na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa TALGWU, Festo Mbakilwa, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wafanyakazi wa chama hicho uliofanyika mkoani Dodoma, ambapo pia viongozi wapya wa chama walichaguliwa.
Mbakilwa amesema ushirikiano kati ya Serikali na TALGWU ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi, akisisitiza kuwa njia bora ya kusimamia haki za wafanyakazi ni kwa pande husika kukaa pamoja na kujadiliana.
“Sisi hatuna ugomvi na Serikali, tunashirikiana na Serikali. Hakuna kitu kizuri kama kusimamia haki ya mfanyakazi kwa kukaa mezani na kujadiliana,” amesema.
Amesema Serikali imekuwa ikishirikiana vyema na TALGWU katika kuhakikisha changamoto na masuala yanayohusu haki za wafanyakazi yanapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Katika hatua nyingine, Mbakilwa amewataka wanachama wa TALGWU kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi bora, waadilifu na wenye uwezo wa kuiongoza chama kwa manufaa ya wanachama, Serikali na chama kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa uchaguzi unapaswa kufanyika kwa kuzingatia katiba ya chama na misingi ya demokrasia, akionya kuwa matumizi ya njia zisizo sahihi yanaweza kusababisha migogoro ndani ya chama.
“Mnapokwenda kuchaguana, mchague kwa njia nzuri na si kwa njia mbaya. Njia nzuri itawaletea kiongozi bora ambaye atakwenda kukisaidia chama na Serikali,” amesema.
Mbakilwa pia amesisitiza umuhimu wa kutatua migogoro ya wafanyakazi kupitia mazungumzo na majadiliano badala ya kukimbilia kutumia sheria katika kila jambo.
Amesema kukaa pamoja na kujadiliana kunaweza kusaidia kupata suluhisho lenye haki na tija kwa pande zote, huku akionya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya sheria yanaweza kuongeza changamoto badala ya kuzitatua.
“Hakuna kitu kizuri kama kusimamia haki ya mfanyakazi kwa kukaa mezani. Ukitaka kusimamia sheria kila wakati, ipo siku sheria inaweza kukutia aibu, kwa sababu siku utakutana na sheria yenye makali,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa TALGWU, Audax Stephano, amesema chama hicho hufanya uchaguzi wa viongozi kila baada ya miaka mitano, huku Mkutano Mkuu ukifanyika kila mwaka kwa mujibu wa katiba ya chama.
Amesema Mkutano Mkuu pia hutoa fursa kwa chama kuwasilisha taarifa mbalimbali, ikiwemo taarifa za mapato na matumizi pamoja na masuala yanayohusu maendeleo na uendeshaji wa chama.
Stephano ameipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao.
Amesema mchakato wa uchaguzi unaendelea vizuri na anaamini utaendelea kuzingatia haki, usawa na misingi ya demokrasia.
“Tunaipongeza Serikali kwa kusaidia wafanyakazi. Wamekuwa wakifanya kazi kwa uhuru na kwa kuzingatia taratibu zilizopo nchini. Zoezi linaendelea vizuri na ninaamini haki na demokrasia zitatumika,” amesema Stephano.



Post a Comment