Tanga
Kamati ya Pamoja ya Ufundi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda (Joint Technical Committee) imekutana Jijini Tanga leo Septemba 30, kujadili hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuliendeleza Jiji la Tanga kuwa Kitovu cha Nishati - Tanga Energy Hub.
Katika kikao hicho, Kamati inajadili hatua zinazofuata katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mafuta ghafi (Refinery), ujenzi wa bomba la kusafirisha bidhaa za mafuta kutoka Tanga, Tanzania hadi Kampala, Uganda, pamoja na ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta na miundombinu ya kupokea na kupakia mafuta (Marine Storage Terminal and Jetty) inayopendekezwa kujengwa katika Bandari ya Tanga.
Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania na Uganda kupitia kuimarisha biashara ya nishati, kuongeza fursa za ajira, kukuza ushiriki wa wazawa katika miradi ya kimkakati kupitia local content, pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu na wananchi watakaonufaika na fursa zitakazotokana na miradi hiyo.
Aidha, kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Uganda katika utekelezaji wa miradi ya pamoja ya nishati, sambamba na kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na biashara katika sekta hiyo.
Kwa nafasi yake ya kijiografia na uwepo wa Bandari ya Tanga, Jiji la Tanga linaendelea kuwa eneo muhimu katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la kimkakati la nishati na biashara kwa nchi zisizo na bandari, ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Uendelezaji wa Tanga kuwa Kitovu cha Nishati unatarajiwa pia kuchochea maendeleo ya miundombinu ya nishati, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa za mafuta, pamoja na kuchangia katika ajenda ya kikanda ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama na yenye gharama nafuu.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Tanzania na Uganda ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kutumia fursa za kimkakati zilizopo katika sekta ya nishati kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa nchi hizo mbili.






Post a Comment