TANROADS YATOA WITO KWA MAMENEJA 26 KUJIANDAA NA MVUA ZA EL NIÑO


......

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) umewataka Mameneja wa mikoa yote 26 nchini kufanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, makalavati na maeneo mengine hatarishi ili kuchukua hatua za haraka kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo pamoja na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.


Mhandisi Besta amesema TANROADS inapaswa kuwa makini kwa kutambua mapema maeneo ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kabla ya mvua kuanza.


Amesema ukaguzi huo ni muhimu kutokana na changamoto zilizowahi kujitokeza katika baadhi ya maeneo wakati wa mvua, akitolea mfano Daraja la Mutikila, ambalo Desemba mwaka jana liliathiriwa na mvua na kusababisha usafiri wa magari na wananchi kukwama.


“Natoa rai kwa mameneja wote wa mikoa 26 waende wakafanye ukaguzi na kuangalia ni namna gani wanaweza kupunguza athari zinazoweza kutokana na mvua za El Niño,” amesema Mhandisi Besta.


Amesema pamoja na Daraja la Mutikila, TANROADS inahakikisha kazi katika madaraja ya Mangungo na Kikombo, pamoja na madaraja mengine yanayotekelezwa katika mradi huo, yanakamilishwa kwa wakati ili yaweze kupitika wakati wa mvua.


Mhandisi Besta pia amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya kazi ili kukamilisha sehemu iliyobaki na kuwawezesha wananchi kunufaika na barabara hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, mradi huo una urefu wa jumla ya kilomita 76 na unatekelezwa kwa awamu mbili.


Amesema awamu ya kwanza inayotekelezwa sasa inahusisha kilomita 25 na imefikia asilimia 67.9 ya utekelezaji.


Kati ya kilomita hizo, kilomita 8.6 ziko upande wa Ntyuka kuelekea Mvumi, huku upande wa Kikombo ukiwa na kilomita 14.4, ikiwemo kilomita tano zinazounganisha barabara hiyo na barabara ya kuelekea Makao Makuu ya Jeshi.


Mhandisi Amani amesema mkandarasi wa mradi huo ni CHICO, ambaye tayari amekamilisha ujenzi wa sehemu kubwa ya barabara ambapo kilomita 23.2 kati ya 25 zimefikia kiwango kinachohitajika.


Amesema kazi kubwa zilizobaki ni pamoja na kujaza tuta la barabara, kuunganisha maeneo ya madaraja na kukamilisha miundombinu ya kupitisha maji katika maeneo ya Mutikila, Mangungo na Kikombo, pamoja na daraja la reli ya MGR.



Amesema TANROADS tayari imeanza kuimarisha maeneo ya madaraja yaliyokuwa yakileta changamoto wakati wa mvua kwa kutumia kifusi, kuimarisha kingo za matuta na kufungua njia za mito ili kuhakikisha watumiaji wa barabara wanaendelea kupita salama.


Kwa mujibu wa Mhandisi Amani, TANROADS inatarajia madaraja ya Mutikila, Mangungo na Kikombo kukamilika na kufikia hatua ya kupitika kabla ya kuanza kwa mvua, hatua itakayosaidia kupunguza usumbufu kwa wananchi na watumiaji wengine wa barabara.




0/Post a Comment/Comments