TANZANIA NA CROATIA ZAZUNGUMZIA KUIMARISHA UHUSIANO NA USHIRIKIANO

******

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulaya wa Jamhuri ya Croatia, Mhe. Gordan Grlić-Radman, jijini New York, Marekani, tarehe 25 Septemba 2026, pembezoni mwa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika mazungumzo hayo, Mawaziri hao wamejadili namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Croatia, hususan katika biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, kilimo na biashara ya kilimo, uchakataji wa mazao ya chakula, utalii, mafunzo ya kidiplomasia na uwakilishi wa heshima wa kibalozi.

Mawaziri hao pia wamebadilishana mawazo kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa, amani na usalama katika maeneo mbalimbali duniani, uhusiano wa Umoja wa Ulaya na nchi nyingine, pamoja na uwezekano wa kusaidiana katika kugombea nafasi katika mashirika ya kimataifa.

Kombo amehimiza wafanyabiashara wa Croatia kuongeza ushiriki wao katika fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania. Pia amependekeza kuimarishwa kwa uwakilishi wa kidiplomasia na kufanyika mara kwa mara kwa mashauriano ya kisiasa kati ya Tanzania na Croatia.

Kwa upande wake, Waziri Grlić-Radman ameeleza utayari wa nchi yake kuendelea kuimarisha mazungumzo na ushirikiano kati ya Tanzania, Croatia na wadau mbalimbali barani Ulaya.








 

0/Post a Comment/Comments