TRA YAKUTANA NA WAZALISHAJI WA SARUJI, WAAHIDI KUZALISHA KWA WINGI KUTOSHELEZA SOKO

*******

Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda umekutana na kufanya mazungumzo na wazalishaji wa Saruji nchini ambao wameahidi kuzalisha bidhaa hiyo kwa wingi kutosheleza soko.

Katika kikao hicho kilichofanyika Septemba 25, 2026 kwenye ofisi za TRA jijini Dar es Salaam wazalishaji hao kwa umoja wao wakiongozwa na viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini Tanzania (CTI) wamesema wamefurahishwa kukutanishwa pamoja na TRA na kueleza kuwa wataendelea kulipa kodi kwa hiari na kuzalisha saruji kwa wingi kulingana na mahitaji ya soko.

Wazalishaji hao kutoka viwanda mbalimbali nchini wameeleza kuridhishwa na huduma za kodi wanazopatiwa na TRA pamoja na elimu ya kodi ambayo imewawezesha kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwaajili ya maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria katika ulipaji kodi na kueleza kuwa watawawezesha wazalishaji hao kuongeza wigo wa uzalishaji na kuwataka wale wanaopata msamaha wa kodi kuutumia vizuri. 

Amesema TRA itaendelea kufuatilia uzalishaji na bei za saruji kuanzia viwandani mpaka kwa wauzaji wadogo ili kuhakikisha kodi stahiki ya Serikali inalipwa.









Mwisho
 

0/Post a Comment/Comments