UBUNGO YAENDELEA KUFANYA USAFI WA MTO GIDE KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO

...   ......

Manispaa ya Ubungo imeendelea kuchukua hatua za mapema za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño, kwa kuendesha zoezi la kusafisha na kuondoa taka katika Mto Gide .

Zoezi hilo limehusisha ushiriki wa Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe. Ally Ibrahim  Hanje, Diwani wa kata ya Mabibo Mhe. Ashura Sengondo, pamoja na watendaji kutoka Idara ya Mazingira ya Manispaa ya Ubungo, kwa lengo la kuhakikisha njia za maji zinakuwa wazi na kupunguza uwezekano wa mafuriko wakati wa mvua zinazotarajiwa.

Hatua hiyo imekuja wakati ambapo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuhusu msimu wa mvua za Vuli wa mwaka 2026, huku maeneo mbalimbali yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Naibu Meya wa Ubungo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu wa mazingira na wananchi katika kuhakikisha mito, mifereji na mitaro inakuwa safi na wazi kabla ya mvua kuanza kunyesha kwa nguvu.

Kwa upande wake, Diwani Ashura Sengondo amewataka wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mito hiyo kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira kwa kuacha kutupa taka kwenye mito, mifereji na mitaro.

Nao wataalamu kutoka Idara ya Mazingira ya Manispaa ya Ubungo wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mito na mifereji, huku wakisisitiza kuwa taka zinazotupwa ovyo zinaweza kuziba njia za maji na kuongeza uwezekano wa maji kujaa katika maeneo ya makazi.

“Usafi wa mito ni jukumu la kila mmoja. Tukishirikiana mapema, tunaweza kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi,” imeelezwa.

           



 

0/Post a Comment/Comments