Na Carlos Claudio, Dodoma
Ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa la Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma umefikia asilimia 55, huku viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wakieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi na watendaji wa UWT leo Septemba 24,2026 jijini. dodoma katika eneo la mradi huo, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Khamis Juma, amesema jengo hilo lina viwango vya kisasa na miundombinu muhimu kwa ajili ya shughuli za chama.
Amesema wajumbe wamepata fursa ya kujionea maendeleo ya ujenzi na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu wanaosimamia mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, amesema mradi huo unatokana na maono ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka wasimamizi kuongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kwa wakati.
Chatanda amesema jengo hilo litakuwa na ukumbi wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watu 500, pamoja na mifumo ya kisasa ikiwemo kiyoyozi (AC), mifumo ya kuzima moto na TEHAMA.
Amesema matarajio ni kukamilisha ujenzi huo ifikapo Februari 5, 2027, ikiwa ni siku ambayo CCM itatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
“Tunatarajia mpaka tarehe hiyo tuwe tumekamilisha ujenzi wa jengo letu kikamilifu,” amesema Chatanda.
Msimamizi wa mradi huo, Msanifu Majengo Lucas Martin,amesema kuwa jengo hilo litakuwa la kisasa lenye ghorofa tano pamoja na ukumbi wa kisasa wa mikutano (auditorium) wenye uwezo wa kuchukua takribani watu 500.
Amesema jengo hilo pia litakuwa na ofisi mbalimbali za chama, zikiwemo za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, pamoja na ofisi za watumishi wengine.
“Mpaka sasa, mradi wetu umefikia asilimia 55 na kazi zinazoendelea zaidi ni za ukamilishaji ikiwemo kupiga plaster, kusawazisha kuta (), na kupaka rangi,” amesema Martin


Post a Comment