VETA YAWAFUNGULIA FURSA VIJANA 784 WENYE ELIMU YA JUU KUPATA UJUZI WA VITENDO


....

Na Carlos Claudio, Dodoma

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeeleza kuwa jumla ya vijana 784 waliomaliza elimu ya juu wamejiunga na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri na kuongeza nafasi zao za kuajiriwa katika soko la ajira.

Hayo yamesemwa leo, Septemba 4, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27 wa Mamlaka hiyo.

Kasore amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa VETA kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta mbalimbali za uchumi, ikiwemo uwekezaji, viwanda, miradi ya kimkakati, madini, utalii, kilimo cha kisasa na usafirishaji.

Amesema ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini umeongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa vitendo, hivyo ni muhimu Watanzania kuandaliwa kushiriki kikamilifu katika nguvu kazi ya taifa.

Kwa mujibu wa Kasore, fursa hizo zinahusisha maeneo mbalimbali kama ujenzi, uendeshaji wa mitambo, huduma za utalii pamoja na matumizi ya teknolojia mpya, hali inayohitaji vijana kuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Amesema VETA inaendelea kupanua wigo wa mafunzo ili kuwapa vijana na wananchi uwezo wa kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi na kujenga uwezo wa kujiajiri.

Katika hatua nyingine, Kasore amesema VETA imeendelea kutoa mafunzo kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa lengo la kuongeza thamani na kuboresha ubora wa kazi zao.

Amesema hadi sasa jumla ya wananchi 4,465 wamefikiwa kupitia programu hizo za mafunzo.

Aidha, katika mwaka wa masomo 2025/2026, VETA ilidahili jumla ya wanafunzi 116,468, ikilinganishwa na wanafunzi 69,377 waliodahiliwa mwaka 2022/2023.

Kasore amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya 65, ambavyo vinajumuisha vyuo 64 vya wilaya na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe.

Amesema kukamilika kwa vyuo hivyo kutaongeza idadi ya vyuo vya Serikali vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi kutoka 80 hadi 145.

Kwa mujibu wa Kasore, mafunzo ya muda mfupi katika vyuo hivyo yanatarajiwa kuanza Oktoba 2026, huku mafunzo ya muda mrefu yakianza Januari 2027.

Amesema Serikali pia imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata mafunzo hayo kwa kugharamia asilimia 80 ya gharama za mafunzo, huku mwanafunzi akichangia asilimia 20.

Katika kuhakikisha makundi maalumu hayabaki nyuma, Kasore amesema zaidi ya watu 80 wenye ulemavu wamepatiwa ufadhili wa asilimia 100 wa mafunzo ya ufundi stadi unaotolewa na Serikali.

Kwa upande wa wanawake, amesema VETA imefikia asilimia 32 ya ushiriki wa wanawake katika mafunzo ya ufundi stadi, huku ikilenga kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 45.

Kasore amesema VETA pia imeendelea kuimarisha uwezo wa wakufunzi wake, ambapo wakufunzi 322 wamejengewa uwezo ndani na nje ya nchi.

Amesema baadhi ya wakufunzi hao wamepata mafunzo katika nchi za Finland, China na India, hususan katika maeneo ya madini, akili bandia (AI) na teknolojia za kisasa.

Aidha, VETA imeshirikiana na viwanda 16 kuwajengea uwezo wafanyakazi 600, huku wajasiriamali 4,963 wakipatiwa mafunzo bure, wakiwemo mama na baba lishe pamoja na wavuvi.

Akizungumza kuhusu fursa hizo, Kasore amewataka Watanzania, hasa vijana na wanawake, kutumia fursa zinazotolewa na VETA kupata ujuzi wa ufundi stadi, akisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi unaendelea kuongeza fursa za ajira na kujiajiri ambazo zinahitaji nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo.

 

0/Post a Comment/Comments