Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amewataka wadau wa Sekta ya Utalii nchini kuendelea kuwekeza katika teknolojia na ubunifu katika kutangaza vyema vivutio vya utalii ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Wito huo ametoa leo 27 Septemba, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani na uzinduzi wa eSimCard; mfumo rasmi utakaosaidia kuwaunganisha watoa huduma za utalii na watalii wa maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
"Kaulimbiu ya mwaka huu inatukumbusha kuwa utalii wa sasa hauwezi kutenganishwa na teknolojia. Watalii wanatumia teknolojia kutafuta taarifa, kuchagua maeneo ya kutembelea, kupanga safari, kufanya booking na kushirikisha uzoefu wao,” amesisitiza Mhe. Chande.
Aidha, amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha uwekezaji unaochochea mageuzi ya teknolojia na uchumi, ubunifu na matumizi ya TEHAMA katika kuendeleza Sekta ya Utalii, ukarimu na kuimarisha uhifadhi hatua iliyosaidia kuongeza tija katika kuimarisha ushindani hususan katika soko la utalii Kimataifa.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha teknolojia inageuka kuwa matokeo ili kusaidia katika ongezeko la watalii zaidi, huduma bora na thamani zaidi kwa Taifa."
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa matumizi ya teknolojia na ubunifu katika Sekta ya Utalii kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitaki kuwa mtazamaji wa mapinduzi ya kidijitali bali inataka kuwa sehemu ya wanaoyaongoza katika ukuaji na maendeleo ya Sekta ya Utalii duniani.














Post a Comment