Makubaliano hayo yanalenga kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa za saratani kwa wanachama wa NHIF.
Mkataba huo umesainiwa Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene C. Isaka, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Zeenat Sulaiman.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Isaka amesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za NHIF kuboresha huduma kwa wanachama wake.
Amesema hatua hiyo pia inalenga kuongeza vituo vinavyotoa huduma za kibingwa kupitia mtandao wa watoa huduma wa Mfuko.
“Tunaboresha wigo na ubora wa huduma zinazopatikana kwa wanachama wetu,” amesema.
Dkt. Isaka amesema makubaliano hayo yanaendana na jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati na kwa usawa.
Kwa upande wake, Dkt. Sulaiman amesema Aga Khan inathamini ushirikiano huo na NHIF.
Amesema taasisi hiyo itaendelea kutumia wataalamu, teknolojia na uzoefu wake katika kutoa huduma za saratani kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wanachama wa NHIF watanufaika na huduma za saratani kwa wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, Mwanza na kliniki 14.
Huduma hizo zinajumuisha tiba ya mionzi pamoja na tiba kwa kemikali.
Wanachama pia watapata nafasi ya kuhudhuria kliniki za saratani kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya NHIF.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza wigo wa vituo vinavyotoa huduma za saratani kwa wanachama wa Mfuko.
Hatua hiyo pia itawawezesha wagonjwa kupata huduma za kibingwa kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu na kutumia teknolojia zinazohitajika katika matibabu ya saratani.











Post a Comment