WASICHANA WASOMESHWE NA WASHAURIWE

Jaji Zephrine Galeba
Jengo la ghorofa kwaajili ya kidato cha tano na sita, Sekondari ya wasichana Mavuno Modal
Mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana Mavuno Modal, Mwl. Glory Herman
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kayanga, Mhashamu Almachius Rweyongeza
Mkurugenzi wa shirika la Mavuno, Charles Bahati
.........

Na Daniel Limbe

ELIMU bora kwa watoto wa kike bado inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na historia yake licha ya jitihada mbalimbali za serikali na wadau wa maendeleo kupambana kila uchao ili kuondoa mtazamo hasi kuwa mwanamke ni chombo cha starehe pekee.

Tawala foatauti zimekuwa na namna ya mbalimbali ya kushughulikia haki za watoto wa kike ingawa bado kundi hilo linakabiliwa na shida na taabu kutokana na kile kinachoitwa mfumo dume.

Ukweli ni kwamba elimu kwa wasichana ni nyenzo muhimu sana kwa taifa lolote duniani iwapo limedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ya ki uchumi na kimaendeleo kutokana na kuwa waaminifu na wenye hofu ya Mungu kuliko wanaume.

Pia wasichana wengi walioelimika wamekuwa chachu kubwa ya amani ya nchi na walezi wema wa familia katika jamii tunamoishi.

Pamoja na ukweli huo, lakini msukumo wa kielimu kwa wasichana bado haujatiliwa mkazo wa kutosha kutoka kwa wazazi na viongozi waliopewa dhamana ya kuhakikisha kundi hili linakombolewa, kutowajibika ipaswavyo kutokana na kuendekeza mila na destuli potofu za kumwandaa binti kuolewa siku za usoni.

"Mavuno Project" ni miongoni mwa taasisi isiyokuwa ya kiserikali iliyoamua kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha wasichana wanapata haki yao ya msingi ya kusoma pasipo vikwazo vinavyodimimiza ndoto zao.

Agost 28 na 29, 2026 shirika hilo limejivunia mafanikio yake kwa kutimiza miaka 10 tangu kuasisiwa kwa shule ya sekondari ya wasichana ya Mavuno Madal, kufanya mahafari ya nane ya kidato cha nne 2026 pamoja na kuzindua majengo mapya ya ghorofa kwaajili kupokea wasichana wanaotarajiwa kujiunga kidato cha tano na sita kwa mhula wa masomo mwaka 2026/27.

Matukio kama haya siyo mageni machoni pa jamii, kwa sababu hufanyika maeneo mbalimbali nchini ispokuwa tunachopaswa kukitazama zaidi ni dhamira ya kumuinua mtoto wa kike katika suala zima la kupata elimu bora.

Kabla ya matukio haya kumalizika, Mgeni rasmi alikuwa Jaji wa Mahakama ya rufani Tanzania, Zephrine Galeba, ambaye alisema ili kumnasua mtoto wa kike katika kisiwa chenye misukosuko na machafuko ya jamii, ni lazima kuzishika amri 10 za binti anayejitambua pamoja na wazazi kusimama kidete na kuwatia moyo watoto wao ili kuzifikia ndoto wanazozitamani siku za usoni.

Jaji Galeba, alisisitiza suala liwe kuwainua wasichana kielimu ikiwa ni pamoja na jamii kutumia muda mwingi kuwasikiliza, kutatua hofu na changamoto zinazowakabili sambamba na kuwapa fursa za ajira badala ya kuwakatisha tamaa kuwa hakuna ajira serikalini.

Ukweli ni kuwa hatuwezi kukataa kuwa elimu ni gharama na kwa nchi yetu wazazi wengi hasa vijijini wanaendesha maisha yao kwa mitaji midogo na kilimo cha jembe la mkono, ingawa maisha yanatofautiana kati ya familia moja na nyingine.

Pia hatuwezi kukataa kuwa hatuna budi kwa muktadha wa uchumi wetu, tabaka la wanawake viongozi, wafanyabiashara na wateknolojia wanapaswa kuwepo na hakuna budi walindwe kwa wivu mkubwa.

Hii ndiyo sababu kila kukicha serikali na wadau wengine wa maendeleo wanaumiza vichwa kuhakikisha zinajengwa shule maalumu kwaajili ya wasichana ili baadaye kuwa na nchi ya wasomi na wanawake waliostaarabika. 

Aidha Jaji Galeba anazitaja amri 10 za binti anayejitambua kuwa ni binti kutooga na mtu yoyote kwa sababu hali hiyo hujenga tabia ya kutoona aibu kuvua nguo kwa mtu mwingine, kutovaa nguo fupi na zenye kubana maana kuchochea ushawishi kwa wanaume, kutoongea na mwanaume yoyote kuhusiana na mapenzi pamoja na kujiepusha kukaa sehemu za faragha na mwanaume yeyote ambaye hamjazaliwa tumbo moja.

Zingine ni kutokubali kupokea zawadi yoyote kutoka kwa mwanaume ambaye si nduguyo, kutolala na mwanaume yoyote kabla ya kuolewa, kutomtembelea mwanaume yoyote asiye ndugu ukiwa pekee yako na kama ni lazima ni muhimu kuwa sehemu ya wazi, kutojiringanisha na wengine ki maumbile au kitabia, kutotamani vipaji na mafanikio ya wengine pamoja na kutorejea nyumbani wakati wa giza.

Kadhalika anawasisitiza wazazi kuwalea vyema watoto wao ili kuwa na la viongozi wenye maadili na walioandaliwa vyema ili kuepuka nchi kukabidhiwa watu wahuni wasiokuwa na maadili wala hofu ya Mungu.

Dhamira ya shirika la Mavuno

Mkurugenzi wa Shirika na Meneja wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Mavuno Modal, Charles Bahati, anasema dhamira ya taasisi hiyo ni kuwa na jamii ya wasichana na wanawake walioelimika na wenye ujuzi mkubwa unaoweza kuchangia maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ushindani wa kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Dhamira hiyo imeisukuma taasisi yake kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 3.3 kwaajili ya ujenzi wa Jengo la ghorofa litakaloweza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano na sita kuanzia mwaka 2026/27.

Hali Kadhalika, amekuwa akitumia muda wake mwingi kuwahimiza watoto wa kike kusoma kwa bidii, kuonyesha nidhamu kwa wakubwa na wadogo pamoja na kujiamini katika ndoto zao.

Kauli hiyo ya Meneja wa shule inaungwa mkono na nukuu ya Mwanafalsafa Farrah Gray inayosema " Jenga ndoto zako wewe mwenyewe, la sivyo mtu mwingine atakuajiri kujenga zake".

Kumbe wasichana bado wanalojukumu la kupambana kuzifikia ndoto zao pasipo kukatishwa tamaa kwa namna yoyote ile ili baadaye wasije kuwa watumwa wa hisia za watu wengine wakiwemo waume zao.

Vile vile Bahati, anarudisha pongezi nyingi kwa viongozi mbalimbali wa kiserikali, kijamii na shule husika kutokana na ushirikiano mkubwa unaotolewa katika uendeshaji wa shule hiyo ambayo imekuwa mkombozi na kimbilio la wananchi walioko vijijini kutokana na taaluma bora inayopatikana.

"Tunaendelea kuboresha miundombinu ya shule yetu, maslahi ya watumishi, kusaidia jamii hasa watoto wa kike wasiokuwa na uwezo wa kugharamia ada pamoja na kuimarisha ushirikiano wetu na taasisi zingine pamoja na serikali kwa ujumla" amesema Bahati.

Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Gloria Herman, anasema elimu kwa mtoto wa kike ni nguzo inayomlinda mwanamke kukabiliana na unyanyasaji, ukatili na kujiamini katika kuwasilisha mawazo na ujuzi wake katika jamii inayomzunguka.

Shule ya sekondari ya wasichana ya Mavuno Modal mbali na mambo mengine imekuwa ikifanya vizuri sana katika matokeo ya kidato cha nne tangu kuanzishwa kwake miaka 10 iliyopita kwa kupata ufaulu wa aslimia 100 na kupokea pongezi mbalimbali kutoka serikalini, wahisani na wadau wengine wa maendeleo.

Ndiyo maana shule hiyo imekuwa mstari wa mbele kuiandaa jamii ya watanzania wa kesho kujitambua, kujiamini, kujithamini na kujipenda ili watakapo kuwa katika jamii, waonekane kuwa ni kikazi chenye maadili na ujuzi uliotokana na malezi bora ya shule hiyo.

Licha ya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma, suala la malezi bado linapewa kipaumbele kwa sababu jamii bora inaamdaliwa leo, hivyo jitihada za jamii, serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu sana katika ulimwengu uliostaarabika.

Mwl. Glory anasisitiza kuwa kuwa elimu ndiyo uwekezaji wenye hazina kubwa katika maisha ya mwanadamu na kwamba watoto wa kike wakielimika mapinduzi ya kifikra,kiuchumi na kisiasa yatafikiwa kwa haraka.

Kauli hii unakwenda sambamba na nukuu ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela aliyosema "Watoto ni hazina ya Taifa 
lolote, tunapowatunza leo, tunajenga dunia bora ya kesho"

Kauli ya Askofu Rweyongeza

Akizungumzia suala zima la elimu kwa watoto wa kike, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kayanga, Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, anajikita katika maadili huku akiitaka jamii kurejea kwenye misingi bora ya malezi kwa watoto badala ya kuziachia taasisi za elimu na dini pekee.

Akinukuu kitabu kitakatifu cha Biblia, anasema "Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa" na kwamba maadili mema ndiyo humfanya mtu kuwa na hofu ya Mungu na kumpenda.

"Huwezi kutaka kuwa na jamii iliyostaarabika iwapo utamnyima elimu mtoto wa kike, kundi hilo ni muhimu sana katika maendeleo endelevu ya Taifa na jamii yetu" alisema.

Vile vile anawahimiza wasichana wahitimu wa elimu ya Sekondari kuziishi ndoto zao na kuendelea kujielimisha kila uchao, kwa kuwa maarifa mengi yamefichika kwenye vitabu vitakatifu vya Biblia, Quran na Magazeti.

"Ni muhimu sana jamii ijenge Utamaduni wa kujisomea maana ndimo kwenye maarifa mengi, niwasihi vijana wasome Magazeti, Biblia na Quran na muhimu watambue kuwa maisha ni hesabu, ukizipiga vibaya unapotea na ukifanya vizuri utaona faida yake" alisema.

Hata hivyo, hakusita kumwaga pongezi zake nyingi kwa Mkurugenzi wa shirika la Mavuno Project kwa kuwaza vyema kusaidia elimu ya watoto wa kike katika jamii ya watu Karagwe na Tanzania kwa ujumla.

Amesema uongozi bora ni kufanya kwaajili ya maslahi mapana ya wengine na si kujilimbikizia kwa manufaa binafsi huku akisisitiza kila mtu anapaswa kuacha alama ya alichokifanya katika jamii kabla ya kutwaliwa na umauti.

"Lazima tujifunze kuacha alama, jiulize wewe umeacha alama gani hata utakapokuwa umekufa ili jamii ikukumbuke kwa wema wako" alihoji Askofu Rweyongeza.

Upo msemo wa Benjamin Franklin usemao "Andika kitu chenye manufaa kusomwa au fanya kitu chenye manufaa kuandikwa.” 

Naibu Katibu mkuu Mipango na Maendeleo wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania( KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Mchungaji Joachim Makori, anakazia juu ya maadili kwa vijana na kuwataka kujiepusha na msukumo wa kidunia unaoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
r
Anasema hakuna njia ya mkato katika maisha, na kwamba vijana wa kike hawana budi kujitambua na kusimama katika maadili mema yanayokubarika katika jamii.

Hivyo kijana ili aweze kufanikiwa katika malengo yake ni muhimu kujengwa katika maadili ikiwemo kuwa na staha, kujistili kwa mavazi yanayo jenga heshima kwa jamii na kuwa na maono ya siku zijazo.

Anawaonya wasichana na maisha ya kuiga mitandaoni badala yake wajinyenyekeze mbele za Mungu na kumlilia katika matanio yao ili aweze kuwafungulia Baraka na kuyapata mafanikio kwa njia halali badala ya kutweza utu wao.

Rai yangu

Haki ya kupata Elimu ni ya msingi sana kwa kila mtu, na inatambuliwa na mikataba ya kitaifa na kimataifa ya Haki za binadamu.

Haki hii inahakikisha kuwa kila mtu ana fursa sawa ya kupata elimu bila unaguzi wa aina yoyote.

Aidha haki ya kupata Elimu imefanywa kuwa haki ya kimsingi ili kuwezesha maendeleo ya mtu binafsi na kuchangia katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Elimu ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye usawa, uhuru na Maendeleo endelevu.

Hivyo, Serikali, Jamii, wahisani na wadau wengine wa maendeleo wanalo jukumu la kuhakikisha utekelezaji wa Haki ya kupata elimu kwa wote unazingatia Tamko la haki za binadamu la umoja wa mataifa na mikataba ya kimataifa ya Haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
 

0/Post a Comment/Comments