******
Watanzania 274 tayari wamenufaika na programu za masomo ya muda mrefu nchini Japan, huku wanataaluma 16 wakielekea nchini humo kwa masomo ya uzamili na mafunzo ya vitendo katika kampuni za Kijapani.
Tanzania na Japan zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika elimu, kupitia fursa zinazolenga kuongeza ujuzi na weledi wa watumishi na wataalamu wa Tanzania.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa JICA nchini Tanzania, Dk. Kuge Katsuya, wakati wa hafla ya kuwaaga wanataaluma hao 16.
Amesema programu hiyo ya ABE Initiative inawapa Watanzania nafasi ya kusoma fani mbalimbali, ikiwemo sera za umma, madini na uhandisi.
Dk. Katsuya amesema masomo ya uzamili huchukua takribani miaka miwili, huku ya uzamivu (PhD) yakichukua karibu miaka mitatu.
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yoichi Mikami, amesema vijana hao ni sehemu muhimu ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo na kuwataka kutumia elimu watakayoipata kwa maendeleo ya Tanzania.
Ofisa Rasilimali Watu Mwandamizi, Margareth Ngondya, amesema mafunzo hayo yanaongeza ujuzi na weledi wa watumishi wa umma, jambo linalosaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
Miongoni mwa wanufaika hao ni Lucy Michael wa BMT, anayekwenda kusoma Global Education na kusema atatumia elimu hiyo kusaidia kuendeleza michezo nchini.

MWISHO.










Post a Comment