AWESO: ELIMU NDIYO UWEKEZAJI WA UHAKIKA

.............

NA: MWANDISHI WETU, PANGANI 

Elimu imetajwa kuwa ndiyo uwekezaji wa uhakika kwa watoto na vijana kutokana na manufaa yake kuwa makubwa.

Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Oktoba 8, 2026, alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Funguni, Jimboni humo.

Aweso amesema, ni vizuri kwa wazazi na walezi, kuweka mkazo katika elimu, kwani uwekezaji huo unalipa katika ujenzi wa maisha ya vijana.

"Leo ukilima unaweza kukosa mavuno, ukifanya biashara pia unaweza kukosa, lakini uwekezaji kwenye elimu una uhakika wa kufanikiwa katika maisha," amesema Aweso.

Aidha, amesisitiza kuwa, ni vizuri wazazi na walezi wakawapa ushirikiano walimu katika kuwalea wanafunzi kimaadili na kitaaluma kwani ushirikiano wa pamoja ni nguzo ya mafanikio.

"Wazazi tuwe kitu kimoja na walimu katika kuwalea watoto. Nidhamu ni muhimu katika  malezi ya watoto, hivyo tutoe ushirikiano kwa walimu ili vijana wetu wafanikiwe kitaaluma na kimaisha. Elimu itamwezesha hata mtoto wa familia maskini kuwa daktari bingwa au hata Rais wa nchi," amesema.

Sambamba na hilo, amesema ataendelea kuweka mkazo zaidi katika sekta ya elimu kwa kushirikiana na baraza la madiwani kwani elimu ndiyo kipaumbele chake namba moja, mbili na tatu.

Katika mahafali hiyo, Aweso ameahidi kutoa pikipiki mbili ili zisaidia kutatua changamoto  ya usafiri shuleni hapo. Mathalani, wanafunzi wanaougua shuleni, kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na nidhamu zao, pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya walimu na wazazi.

Vilevile, Aweso ameahidi kutoa vifaa vya michezo na shilingi milioni kumi ili ziwezeshe ukarabati wa ofisi ya walimu na kununua samani za kisasa ili walimu wafanye kazi katika mazingira mazuri zaidi.

Pia, ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa chakula kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne ili wapate chakula watakapoanza mitihani ya taifa inayotarajia kuanza Oktoba 19, 2026.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Nassoro Gamba, alimshukuru Aweso kwa kuwa bega kwa bega na shule hiyo kwani kumesaidia kuongeza ufaulu.

Katika shukrani zake, Gamba alimshukuru Mbunge huyo kwa kuwezesha ununuzi wa jenereta la shule, ujenzi wa maabara ya kompyuta na vifaa vyake bila kusahau ujenzi wa mabweni na madarasa.

Katika hafla hiyo, Aweso aliambatana na viongozi wengine wakiwemo, Mkuu wa wilaya ya Pangani, Mwanaidi Rajabu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Elikana Zabron, Katibu Tawala wa wilaya, Ester Gama na viongozi wengine wa Chama na serikali.







 

0/Post a Comment/Comments