Na Mwandishi wetu, Geita
RAIS wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini Tanzania (FEMATA) John Wambura Bina, amesema madini ya vito ya Tanzanite yanapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa, kwani ni madini adimu ambayo kwa hapa duniani sehemu yanapopatikana ni Tanzania pekee.
Rais Bina ameeleza hayo mbele ya Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Lameck Nchemba, kwenye hitimisho la maonyesho ya tisa ya teknolojia ya madini iliyofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan Manispaa ya Geita.
Amesema Serikali inapaswa kuona namna ambayo Tanzanite inakuwa na upendeleo maalum na kuboreshwa kwa kuanzia kwenye sheria, kanuni na utaratibu.
“Tanzanite ni mtoto yatima, inayopatikana Tanzania peke yake hapa duniani hivyo inapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa,” amesema Rais Bina.
Amesema wanapaswa kuilinda Tanzanite kwa nguvu zote kwani majasusi wanaweza kufanya hujuma kwa kutengeneza kashfa hadi soko lake likashuka.
“Tuweke timu maalum ambayo itaipa kipaumbele Tanzanite kuhakikisha inapata kipaumbele kwa wivu mkubwa,” amesema Rais Bina.
Hata hivyo, Rais huyo wa FEMATA Bina, ameipongeza Serikali kwa namna wanavyokaa mezani na kuzizungumzia changamoto za sekta hiyo na kuzitatua.
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitusikiliza wachimbaji kupitia kiranja wetu Waziri wa Madini Anthony Peter Mavunde,” amesema Rais Bina.
Post a Comment