Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias John Ndejembi, amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali kuhakikisha mifumo yao inasomana na kubadilishana taarifa ili kuondoa urasimu na kurahisisha upatikanaji wa huduma na fursa kwa wananchi, hususan vijana.
Akizungumza katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, kilichofanyika katika Viwanja vya CCM Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, Ndejembi amesema agizo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuunganisha mifumo ya Serikali ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Ametolea mfano Wizara mbili zinazoshughulikia masuala ya vijana, ambazo zimebuni mifumo tofauti isiyosomana, na kuzitaka kushirikiana kuhakikisha vijana wananufaika na fursa za ajira, mafunzo ya vitendo na uwezeshaji wa kiuchumi.
Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza kuendelezwa kwa mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, VVU na UKIMWI pamoja na umaskini, huku akiwaagiza viongozi kusimamia kwa uadilifu miradi ya maendeleo iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kuenzi misingi ya amani, umoja, uzalendo na uwajibikaji iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuhamasisha maendeleo na ushiriki wa vijana katika shughuli za kiuchumi, huku Kiongozi wa Mbio hizo Kitaifa, Wazo Mwang’onda, akieleza kuwa wananchi wamepongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuomba kuongezwa kwa fursa za uwezeshaji wa vijana na wanawake.
Makamu wa Rais amehitimisha mbio hizo akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho yaliyoenda sambamba na kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa na Maonesho ya 26 ya Wiki ya Vijana Kitaifa.









Post a Comment