BODABODA, BAJAJI WATEMBELEA MTUMBA KABLA YA UZINDUZI WA RAIS SAMIA

.........

 Na Carlos Claudio, Dodoma.

Waendesha bodaboda, bajaji  nchini wametembelea Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kufahamu huduma zinazotolewa na ofisi mbalimbali za Serikali, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa mji huo unaotarajiwa kufanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho, Oktoba 30, 2026.

Ziara hiyo iliyofanyika leo, Oktoba 29, 2026, imeongozwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Bodaboda na Bajaji Tanzania, Saidi Kagomba, ambaye amesema ni muhimu kwa waendesha vyombo hivyo vya usafiri kufahamu majukumu ya taasisi za Serikali na namna wanavyoweza kupata huduma zake.

Kagomba amesema wameamua kutembelea mji huo kabla ya uzinduzi ili kupata uelewa wa shughuli zinazofanyika katika majengo mbalimbali, pamoja na kufahamu namna huduma hizo zitakavyoweza kuwafikia wananchi, hususan wale wanaojishughulisha na sekta ya usafirishaji.

Amesema ziara hiyo imelenga kutembelea majengo matano ya Serikali yanayohusiana na shughuli zao za kila siku, yakiwamo ya Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Ndani, wizara inayoshughulikia masuala ya vijana, Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Uchukuzi.

Amesema wameona ni muhimu kupata maelezo kutoka kwa wataalamu kuhusu majukumu ya ofisi hizo ili waweze kufahamu maeneo ya kupata msaada na huduma wanazohitaji katika shughuli zao za kiuchumi.

Kuhusu Wizara ya Maji, Kagomba amesema huduma ya maji ni muhimu kwa maisha ya wananchi, wakiwamo waendesha bodaboda, bajaji na maguta, ambao wanahitaji maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya nyumbani na katika shughuli zao za kila siku.

"Kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wanatarajia kufahamu namna Serikali inavyoweza kusaidia kuboresha mazingira ya shughuli zao, ikiwamo uwezekano wa kuanzisha vituo vya kisasa vya bodaboda na bajaji vinavyokidhi mahitaji ya waendesha vyombo hivyo, " Amesema.

Ameongeza kuwa Wizara ya Uchukuzi ni muhimu kwao kutokana na shughuli zao kuhusisha usafirishaji wa abiria, hivyo wanahitaji kufahamu taratibu za kisheria zinazohusiana na usafirishaji, ikiwamo masuala ya leseni na huduma nyingine zinazowahusu.

Aidha, amesema wameona umuhimu wa kufahamu namna ya kupata msaada kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na taasisi nyingine za Serikali pale wanapokumbana na changamoto zinazohitaji uingiliaji wa mamlaka husika.

Akizungumza na kundi hilo, Fred Kaduma kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, amesema majengo ya Mji wa Serikali Mtumba yamekusudiwa kuhudumia watumishi wa Serikali, viongozi pamoja na wananchi wa makundi mbalimbali.

Kaduma amesema ofisi hizo hazijajengwa kwa ajili ya viongozi na watumishi pekee, bali ni sehemu ya huduma za umma ambazo wananchi wanapaswa kuzifahamu na kuzitumia kulingana na mahitaji yao.

" Ofisi ya Waziri Mkuu ina dhamana ya kuratibu uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba, huku akiwakaribisha wananchi kutembelea eneo hilo na kupata maelezo kuhusu shughuli zinazofanyika katika majengo mbalimbali, "Amesema.

Kwa upande wake, Paul Frank Nyongo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, amewapa waendesha bodaboda, bajaji na maguta maelezo ya awali kuhusu mji huo, akieleza kuwa eneo walilolitembelea ni sehemu ya mradi mkubwa wa Mji wa Serikali Mtumba.

Nyongo amesema ziara hiyo ni fursa kwa wananchi kufahamu historia ya mji huo, namna wazo lake lilivyoanza na hatua zilizofikiwa hadi maandalizi ya uzinduzi unaotarajiwa kufanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho.

Ziara hiyo imefanyika wakati maandalizi ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba yakielekea kukamilika, huku tukio hilo likitarajiwa kuhusisha uzinduzi wa majengo ya Serikali pamoja na barabara zilizojengwa ndani ya eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

0/Post a Comment/Comments