CBE KUFUNGUA JUKWAA LA BIASHARA NA UCHUMI MWANZA


 ********

Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE) kinatarajia kuwakutanisha wadau wapatao 300 kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani katika Kongamano la Saba la Biashara na Maendeleo ya Uchumi, litakalofanyika jijini Mwanza kwa lengo la kujadili mikakati ya kukuza biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa la kujadili namna ubunifu, matumizi ya teknolojia, upatikanaji wa masoko na urasimishaji wa biashara vinavyoweza kutumika kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushindani katika soko.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Oktoba 16, 2026, Mkuu wa CBE, Prof. Edda Tandi Lwoga, amesema mwaka huu kongamano hilo litafanyika Mwanza kwa mara ya kwanza, likitarajiwa kufunguliwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo.

Amesema mkutano huo utashirikisha wafanyabiashara, wanasheria, watafiti, wanafunzi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali, ambao watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazokwamisha ukuaji wa biashara pamoja na fursa zinazoweza kuendelezwa.

Kwa mujibu wa Prof. Lwoga, miongoni mwa ajenda muhimu ni kujenga biashara zinazoweza kuhimili mabadiliko ya soko, kutumia teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kuimarisha matumizi ya takwimu ili kuwezesha maamuzi yenye tija.

Amesema pia kongamano hilo litatoa nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu uwekezaji, masoko na mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wajasiriamali, hususan biashara ndogo na za kati, ambazo ni sehemu muhimu katika shughuli za kiuchumi.

“Tunatarajia kupata mawazo na uzoefu kutoka kwa wadau wenye mitazamo tofauti, jambo litakalosaidia kubaini njia bora za kuendeleza biashara na kuimarisha maendeleo ya uchumi,” amesema Prof. Lwoga.

Ameeleza kuwa ushiriki wa wadau kutoka Finland, China, Afrika Kusini, Indonesia na Malaysia, miongoni mwa wengine, unatarajiwa kuongeza wigo wa majadiliano na kuwezesha washiriki kujifunza mbinu zinazotumika katika mazingira tofauti ya biashara.

Amesema CBE imekuwa ikifanya tafiti na kutoa mchango katika kuwawezesha wadau wa biashara nchini, ikijikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo biashara za mipakani, upatikanaji wa masoko kwa biashara ndogo na za kati, kilimo cha kibiashara na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo katika maeneo husika.

Ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo, matokeo ya tafiti, ubunifu na mijadala kuhusu sera yatajadiliwa kwa lengo la kupata mapendekezo yanayoweza kusaidia kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Prof. Lwoga amewahimiza wafanyabiashara, wanafunzi, watafiti na wadau wengine kujitokeza kushiriki kongamano hilo, akieleza kuwa litakuwa fursa ya kuongeza maarifa, kuimarisha ushirikiano na kujenga mitandao ya kibiashara na uwekezaji.


0/Post a Comment/Comments