Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt Rogers Shemwelekwa amekabidhi ofisi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Warda Abeid Maulid ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo baada ya kukamilisha mchakato wa kuteua wakurugenzi wa Halmashauri.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Oktoba 02, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Idara za Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, viongozi wa chama na wa taasisi zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati akikabidhi ofisi hiyo, Dkt Shemwelekwa amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kumuamini katika kipindi chote alichohudumu kama Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha hadi kuwa Manispaa.
Amesema, aliweza kuboresha Manispaa ya Kibaha kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuweza kujenga miradi ya kimkakati kupitia mapato ya ndani na tayari kuna miradi imekamilika na kuna mingine inaendelea na ujenzi.
"Hadi kufikia tarehe 30 Septemba tayari tumeshafikia asilimia 50, ya ukusanyaji wa mapato na huwa ikifika Mwezi Desemba tunakuwa tumefika asilimia 100 na miezi iliyobaki ni kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo tunaenda kujenga miradi ya kimakati na kuwasogezea huduma karibu wananchi," amesema
Dkt Shemwelekwa amewashukuru baraza la madiwani kwa ushirikiano alioupata kutoka kwao katika kipindi chote, viongozi wa chama cha mapinduzi na wakuu wa taasisi mbalimbali ambapo waliweza kushirikiana kwa moyo mmoja.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda amesema, anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa majukumu mapya ndani ya Manispaa ya Kibaha.
Amesema, amekuja Kibaha kuendeleza pale ambapo Mkurugenzi aliyepita ameyafanya, na ameahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu mapya aliyopewa na Mhe. Rais.
Amesema, anaomba ushirikiano kutoka kwa wakuu wa Idara , ofisi ya Mkuu wa Wilaya, viongozi wa dini na viongozi wa Taasisi mbalimbali.
Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Mhe. Aziza Adinani Mruma amempongeza Dkt Rogers Shemwelekwa kwa mazuri yote aliyoyafanya ndani ya Manispaa ya Kibaha na wanamtakia majukumu mema huko aendako.
Amesema, Dkt Shemwelekwa ameweza kuwa na ushirikiano mzuri na Baraza la madiwani na wakuu wa idara jambo ambalo liliweza kufanikisha yale mazuri yote yaliyofanyika kwa kipindi kifupi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwl Mwajuma Amiri Nyamka amesema anampongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Warda kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais kwahiyo wanamkaribisha na watampa ushirikiano katika kila hatua.
Amesema, wanaamini watapata ushirikiano wa kutosha kkwa Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa Ilani kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa mpya.








Post a Comment