HASMA HAMISI AAHIDI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NA BARABARA CHAMWINO

.........

Mgombea ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia Chama cha United Democratic Party (UDP), Hasma Judi Hamisi, ameahidi kuishauri serikali kuboresha huduma za afya, upatikanaji wa dawa katika zahanati pamoja na miundombinu ya barabara, akisema hatua hizo zitasaidia kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo hilo.

Hasma amesema iwapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi bungeni, atahakikisha anafikisha kwa serikali changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta ya afya na miundombinu, ili zipatiwe ufumbuzi.

Amesema moja ya vipaumbele vyake itakuwa kuhakikisha zahanati zinakuwa na upatikanaji wa dawa, huduma za afya ya mama na mtoto zinapatikana, pamoja na kuimarishwa kwa huduma za afya kwa wazee na upatikanaji wa bima ya afya kwa kundi hilo.

Katika hatua nyingine, Hasma amesema kuboreshwa kwa barabara ni muhimu ili kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi kwa wananchi, akibainisha kuwa baadhi ya barabara alizopitia haziko katika hali nzuri, hasa linapokuja suala la upitikanaji wake kwa nyakati tofauti za mwaka.

Amesema ataitaka serikali kuzingatia maboresho ya barabara hizo ili ziweze kupitika mwaka mzima, bila kuathiriwa na changamoto za mvua au ukame.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UDP Taifa, Saumu Rashid, amemtaka Hasma kuweka mbele mawasiliano ya mara kwa mara na wananchi na kusikiliza kero zao kabla ya kushiriki vikao vya Bunge, ili aweze kuziwasilisha na kuzitafutia ufumbuzi.

Saumu amesema mwakilishi wa wananchi anapaswa kutanguliza mahitaji ya wananchi anaowaongoza badala ya kuzungumzia mambo yanayotokana na mawazo yake binafsi bila kuzingatia changamoto zinazowakabili wapiga kura wake.

Aidha, amesema UDP itaendelea kumsimamia Hasma ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matarajio ya wananchi wa Chamwino.

Ameongeza kuwa, endapo Hasma ataingia bungeni, atakuwa na jukumu la kusimamia masuala yanayolenga kuinua uchumi wa wananchi wa Chamwino na kuhakikisha changamoto zao zinapata uwakilishi katika ngazi za maamuzi.

Na Carlos Claudio, Dodoma
 



0/Post a Comment/Comments