******
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeweka mikakati mipya ya kuongeza urejeshaji wa mikopo inayodaiwa kufikia takribani Sh800 bilioni, ikiwalenga zaidi wanufaika wanaofanya shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi.
Mikakati hiyo inalenga kuhakikisha fedha zinazorejeshwa zinaendelea kutumika kufadhili wanafunzi wengine wanaohitaji mikopo ya elimu ya juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, amesema hayo Oktoba 12, 2026, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya bodi hiyo katika kipindi cha miaka mitano.
Amesema changamoto ya ajira na kutokuwa na kipato cha uhakika kwa baadhi ya wahitimu imeifanya bodi kubuni njia zinazowawezesha wanufaika kurejesha mikopo kulingana na uwezo wao wa kifedha.
Dk. Kiwia amesema kuanzia mwaka wa fedha 2005/2006 hadi Juni 2026, HESLB imekusanya Sh1.91 trilioni kati ya Sh2.77 trilioni za mikopo iliyofikia muda wa kurejeshwa, sawa na asilimia 69.
Amesema makusanyo yameongezeka kutoka Sh177 bilioni mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh194 bilioni mwaka 2024/2025.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, makusanyo yalifikia Sh235.5 bilioni, sawa na asilimia 107 ya lengo la Sh220 bilioni.
Hatua hiyo imeongeza uwezo wa bodi kuendeleza ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya juu.
Wakati huohuo, Serikali imetenga Sh1.06 trilioni kwa mwaka wa masomo 2026/2027 kwa ajili ya kugharimia wanafunzi wasiopungua 300,000.
Kiasi hicho ni ongezeko kutoka Sh916.7 bilioni zilizotengwa mwaka uliotangulia.
Dk. Kiwia amesema mwaka wa masomo 2025/2026, wanafunzi 289,932 walinufaika na mikopo, huku bajeti ya mwaka huu ikiongezeka kwa asilimia 15.6.
Akizungumzia ugawaji wa mikopo kwa mwaka huu, amesema awamu ya kwanza iliyotangazwa Oktoba 10, 2026, ilihusisha wanafunzi 165,775 waliopangiwa mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh535.7 bilioni.
Amesema wanafunzi 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wamepangiwa Sh246.88 bilioni, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh22.9 bilioni.
Aidha, wanafunzi 873 wamepangiwa ruzuku ya Sh4.5 bilioni kupitia Samia Scholarship.
Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, 79,115 wamepangiwa mikopo ya Sh252.4 bilioni.
Wanafunzi wengine 1,554 wa stashahada wamepangiwa Sh3.8 bilioni, huku wanufaika 926 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Sh5.1 bilioni.
Katika kipindi cha miaka mitano, HESLB pia imepanua wigo wa ufadhili kwa kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada mwaka wa masomo 2023/2024.
Vilevile, bodi imeongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kutoka Sh8,500 hadi Sh10,000 kwa siku.
Katika kuboresha huduma, HESLB imeimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali ikiwemo OLAMS, SIPA, HESLB App na DiDiS.
Pia, bodi imeanzisha mifumo saidizi ya akili unde, Bwanaboom na Bibiboom, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa na majibu kuhusu huduma za mikopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwaji wa Mikopo wa HESLB, CPA George Mziray, amesema bodi inaendelea kutumia kampeni za #Fichua na #Kiduchu Fresh Tunasonga kuongeza makusanyo.
Amesema kampeni ya #Kiduchu Fresh Tunasonga inalenga kuwapa nafasi wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo kwa kiasi kinachoendana na uwezo wao.
Ameeleza kuwa mkakati huo unawalenga zaidi wanufaika wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Sabato Kosuri, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuelimisha umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma.



Post a Comment