*******
NA MWANDISHI WETU
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepokea cheti cha kimataifa cha ubora cha ISO 9001:2015, hatua inayotarajiwa kuimarisha ufanisi, uwazi na ubora wa huduma zake, ikiwamo utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia,Akizungumza leo katika hafla ya kukabidhiwa cheti hicho.Akizungumza leo katika hafla ya kukabidhiwa cheti hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema bodi hiyo inaendelea kuboresha mifumo yake ya utoaji huduma kwa kutumia teknolojia ya kidijitali ili kupunguza muda wa kutuma fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaostahili kutoka siku moja au mbili hadi sekunde mbili.
Amesema HESLB inapanga kuunganisha mifumo yake na kampuni za simu za mkononi ili kuwawezesha wanafunzi kupokea fedha zao papo hapo baada ya taratibu zote zinazohitajika kukamilika.
“Kwa sasa tunatuma fedha ndani ya siku moja au mbili baada ya taratibu zote kukamilika. Hata hivyo, haturidhishwi na muda huo. Tunataka kuunganisha mifumo yetu na kampuni za simu ili wanafunzi waweze kupokea fedha zao papo hapo, ndani ya sekunde mbili,” amesema Dkt. Kiwia.
Amesema bodi hiyo imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia, ambapo wanafunzi sasa wanaweza kuomba mikopo, kuhakiki taarifa zao, kufuatilia akaunti na kuhamisha fedha kwa kutumia simu janja.
Ameeleza kuwa maendeleo hayo ni tofauti na hali ya zamani ambapo HESLB ilitegemea taratibu za karatasi zilizohitaji maandalizi makubwa katika mchakato wa uombaji mikopo. Aidha, amesema mifumo ya bodi hiyo tayari imeunganishwa na majukwaa ya benki ili kurahisisha huduma kwa wanufaika.
Dkt. Kiwia amesema HESLB imewasaidia wanafunzi zaidi ya milioni moja nchini kwa kutoa mikopo yenye thamani ya karibu Sh trilioni tisa, akibainisha kuwa fedha hizo ni uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu na maendeleo ya taifa.
Amesema uwekezaji huo unawawezesha Watanzania kupata elimu ya juu na kuongeza ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali za uchumi.
“Sh trilioni tisa ni kiasi kinachoweza kulinganishwa na uwekezaji katika Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), lakini uwekezaji wetu ni katika rasilimali watu,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa cheti hicho, Dkt. Kiwia amesema kukipata ni hatua muhimu katika kuimarisha imani ya wanafunzi, taasisi za elimu ya juu, Serikali na wadau wengine kuhusu ubora, uwazi na ufanisi wa huduma zinazotolewa na bodi hiyo.
Amesema cheti hicho kinahusisha makao makuu ya HESLB, ofisi ya Zanzibar na ofisi za kanda za Arusha, Mbeya, Mwanza na Mtwara, hatua inayolenga kuhakikisha viwango vya usimamizi wa ubora vinafuatwa katika maeneo yote ya utendaji.
Ameongeza kuwa bodi hiyo imeanza maandalizi ya kupata cheti cha ISO 27001 kinachohusu usimamizi wa usalama wa taarifa, huku ikipanga pia kufuata kiwango cha ISO 37001 kinachohusu mifumo ya usimamizi wa kupambana na rushwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, ameipongeza HESLB kwa kupokea cheti hicho, akisema kitasaidia kuimarisha mifumo ya taasisi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi Akimzungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam.Dkt. Katunzi amesema kupokea cheti ni hatua ya mwanzo, huku kukidumisha kukihitaji taasisi kuendelea kutimiza matakwa ya kiwango husika, kufuatilia utendaji na kuhakikisha mifumo yake inafanya kazi kwa ufanisi.
“Kupata cheti ni hatua moja, lakini kukidumisha ni hatua nyingine. Lazima muendelee kutimiza matakwa yake, kufuatilia utendaji na kuhakikisha mifumo inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.
Ameeleza kuwa kiwango cha ISO 9001:2015 kinatumika katika taasisi za aina na ukubwa tofauti kwa lengo la kuboresha kuridhika kwa wateja, kuongeza tija na kuimarisha ufanisi wa kiutendaji.
Amesema kiwango hicho kina umuhimu mkubwa kwa HESLB kutokana na jukumu lake la kubaini wanafunzi wanaostahili mikopo na kusimamia utoaji wa fedha hizo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Dkt. Katunzi amehimiza HESLB kuendelea kutafuta vyeti vingine vya kimataifa, huku akizitaka taasisi za umma na binafsi kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa ili kuboresha huduma na kuimarisha weledi.
Amesema juhudi hizo zinaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhimiza ufanisi, weledi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.














Post a Comment