INADES YAWEKA MKAZO KUSHIRIKISHA WAKULIMA KATIKA TAFITI NA UBUNIFU WA KILIMO EKOLOJIA

....

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Shirika la Inades Formation Tanzania limesema ushirikishwaji wa wakulima katika tafiti na ubunifu ni muhimu katika kuhakikisha matokeo ya tafiti yanaendana na mahitaji halisi ya jamii na kuwa endelevu.

Akizungumza katika Kongamano la Vijana la Kilimo Ikolojia Tanzania 2026, Mshauri wa Kitengo cha Makuzi kutoka Inades Formation Tanzania, Michael Kiwele, amesema shirika hilo limeendelea kuwa mdau muhimu wa kilimo ikolojia nchini, likilenga kuwawezesha vijana kuongoza mabadiliko kuelekea kilimo na mifumo endelevu ya chakula.

Kiwele amesema Inades inatekeleza shughuli zinazolenga uhifadhi wa mazingira, kilimo endelevu pamoja na ufugaji unaozingatia ikolojia, huku ikihakikisha makundi mbalimbali, yakiwemo vijana, wanawake na wanaume, yanashirikishwa.

Amesema katika programu mbalimbali zinazotekelezwa na Inades, vijana hushirikishwa kwa kiwango cha kati ya asilimia 30 hadi 50, hatua inayolenga kuhakikisha wanakuwa sehemu muhimu ya mabadiliko katika sekta ya kilimo.

Aidha, amesema kupitia kongamano hilo, Inades imeshiriki katika majadiliano yaliyolenga kuangazia umuhimu wa kuwashirikisha wakulima katika tafiti na ubunifu kuanzia hatua ya kuibua tatizo, kufanya utafiti, kutekeleza matokeo hadi kupata mrejesho kuhusu mafanikio ya utafiti huo.

“Ili kuwe na tafiti zinazoshirikisha jamii vizuri na kuwa na matokeo makubwa na endelevu, ni muhimu mkulima au mtumiaji wa mwisho wa utafiti ashirikishwe kuanzia hatua ya kuibua tatizo hadi kwenye matokeo na hatua ya kutoa mrejesho.”

Kiwele amesema ushirikishwaji huo unasaidia kuhakikisha tafiti na ubunifu unaofanyika unalenga changamoto halisi zinazowakabili wakulima na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa Inades Formation Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, wakulima na watunga sera katika kuendeleza kilimo ikolojia nchini.

Amesema shirika hilo pia linafanya ushawishi na uchambuzi wa sera kwa lengo la kuhakikisha uzoefu, maarifa na mahitaji ya wakulima yanafika katika mijadala ya kisera na kuchangia maboresho ya sera na utekelezaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.
 

0/Post a Comment/Comments