🍅 🍅*KAMATI YA BUNGE YAKIRI KUONA MAGEUZI YA KIUTENDAJI TAWA*

.........

📍Yaridhishwa na kasi ya makusanyo, uboreshaji miundombinu

Na Beatus Maganja, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa mageuzi ya kiutendaji hususan katika ukusanyaji wa mapato, ukuaji wa utalii na uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya uhifadhi.

 Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 13, 2026 jijini Dodoma wakati Kamati ikipokea taarifa ya utendaji wa Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo iliyowasilishwa na Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb), amesema mabadiliko yanayoonekana TAWA ni makubwa huku akitaja ukusanyaji wa mapato kuwa miongoni mwa maeneo yaliyofanya vizuri. “Kwa upande wa TAWA, Mheshimiwa Waziri tunawapongeza. Mabadiliko ni makubwa, hasa katika makusanyo ya fedha. Kwa kweli wanafanya vizuri,” amesema.

Mhe. Mnzava pia amepongeza hatua za kupanua wigo wa utalii kutoka uwindaji wa kitalii hadi aina nyingine za utalii akisisitiza juhudi hizo ziendelezwe. “Tumeona kutoka kwenye uwindaji wa kitalii mpaka aina nyingine ya utalii. Kwa hiyo ni msisitizo wetu kuwa jitihada hizi kwa upande wa TAWA ziendelee,” ameongeza.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo, Kamishna Kabange amesema TAWA ilikusanya Shilingi bilioni 92.28 katika mwaka wa fedha 2025/26 sawa na asilimia 91.79 ya lengo la Shilingi bilioni 100.53. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, Mamlaka imekusanya Shilingi bilioni 29.35, sawa na asilimia 94 ya lengo la kipindi hicho, huku lengo la mwaka likiwa kukusanya Shilingi bilioni 124.87.

Katika utalii na uwekezaji, idadi ya watalii wa picha ilifikia 270,823 mwaka 2025/26 huku vitalu vyenye wawekezaji vikiongezeka kutoka 95 hadi 98. Mikataba saba ya uwekezaji kupitia mfumo wa uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas -SWICA) imesainiwa na kuchangia Shilingi bilioni 21.3 sawa na asilimia 23.1 ya mapato yote ya Mamlaka sambamba na juhudi za kuboresha miundombinu na kutangaza vivutio vya utalii.

Kwa upande wa uhifadhi, TAWA imeendelea kuimarisha doria na matumizi ya teknolojia katika kulinda rasilimali za wanyamapori na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. 

Hatua hizo zinajumuisha matumizi ya ndege nyuki, vifaa vya GPS, ufuatiliaji wa makundi ya tembo pamoja na ujenzi wa uzio wa umeme wenye urefu wa kilometa 104 katika Pori la Akiba Maswa.

Mafanikio hayo yanaakisiwa pia katika manufaa kwa wananchi, ambapo TAWA kwa kushirikiana na wadau imechangia Shilingi bilioni 1.36 katika miradi ya maendeleo ya jamii ikiwemo elimu na afya.

 Aidha, ukuaji wa utalii na uwekezaji unaendelea kufungua fursa za ajira, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka hifadhi, huku ongezeko la mapato likiimarisha mchango wa sekta ya wanyamapori katika mapato ya Serikali na maendeleo ya Taifa.

Katika mwaka wa fedha 2026/27, TAWA inalenga kuendeleza kasi hiyo kwa kuongeza mapato, kuboresha miundombinu na huduma za utalii, kuimarisha udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uhifadhi ili rasilimali za wanyamapori ziendelee kuwa chanzo cha manufaa kwa jamii na uchumi wa Taifa.

0/Post a Comment/Comments