MAANDALIZI YA UZINDUZI WA MJI WA SERIKALI MTUMBA YAKAMILIKA - KITILA

......

Na Carlos Claudio, Dodoma

Serikali imeridhishwa na maandalizi ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, unaotarajiwa kufanyika kesho, Oktoba 30, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameeleza kuridhishwa kwake na maandalizi hayo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi leo, Oktoba 29, 2026, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi.

Akiwa katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo amekagua maeneo mbalimbali yatakayotumika katika hafla ya uzinduzi, yakiwemo geti kuu la kuingilia Mji wa Serikali, eneo la uwekaji jiwe la msingi la barabara za lami, eneo la uwekaji jiwe la msingi la majengo ya Serikali pamoja na Uwanja wa Mashujaa, ambako hafla hiyo kuu itafanyika.

Prof. Mkumbo amepongeza hatua iliyofikiwa katika maandalizi hayo na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo, akilitaja kuwa la kihistoria na lenye umuhimu mkubwa kwa taifa.

Kwa niaba ya kamati ya maandalizi, imeelezwa kuwa shughuli za hafla hiyo zitaanza usiku wa leo kwa upigaji wa fataki, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kusherehekea uzinduzi huo.

Kwa mujibu wa ratiba, kesho kutakuwa na shughuli kuu tatu, ambazo ni uzinduzi wa barabara za lami, uzinduzi wa jengo la Utumishi wa Umma kwa niaba ya majengo mengine ya Serikali, na mkutano wa kuzungumza na wananchi katika viwanja vilivyoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo.

Hafla hiyo itahudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa pamoja na mgeni maalumu, Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço.

Uzinduzi huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuimarisha shughuli za kiutawala jijini Dodoma kwa kuziweka Wizara na Taasisi za Serikali katika eneo moja lenye miundombinu ya kisasa.

Mradi wa Mji wa Serikali Mtumba ni alama muhimu ya maendeleo ya kiutawala nchini, ukiwa na majengo ya kisasa ya ofisi na barabara za lami zinazolenga kurahisisha utoaji wa huduma, kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma.

Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo aliambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi; Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko; Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Paul Sangawe, pamoja na maafisa wengine wa Serikali.


 

0/Post a Comment/Comments